HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 8, 2026

MIEZI SITA JELA KWA KUZUSHA KUIBIWA NYETI - SUMBAWANGA



VURUGU ZA “KUIBIWA NYETI” ZATINGISHA RUKWA, WAWILI WAFUNGWA MIEZI SITA JELA

Na Mwandishi Wetu, Rukwa

SIKU za hivi karibuni kumeshuhudiwa taharuki iliyopelekea vurugu na kukosekana kwa amani katika baadhi ya maeneo nchini, ikiwemo Mkoa wa Rukwa, kufuatia madai ya kuzushwa kuhusu kuibiwa kwa viungo vya siri.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa lilifanya msako Aprili 6, 2026 katika Wilaya ya Sumbawanga na kufanikiwa kuwakamata vijana saba waliodai kuwa wameibiwa nyeti zao. Vitendo hivyo vilichochea wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuwashambulia watu wasio na hatia.

Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa alisema kuwa vijana wawili kati ya waliokamatwa, Haruni William Mengo (24), mkazi wa Kalambazite na Isack Simon Kaniki (19), mkazi wa Mshani, wamefikishwa mahakamani na kutiwa hatiani kwa tuhuma hizo.

Mahakama ya Mwanzo Kipeta, Wilaya ya Sumbawanga, chini ya Hakimu Wiligisi Mbunda, Aprili 8, 2026, iliwahukumu wawili hao kutumikia kifungo cha miezi sita jela kila mmoja.

Ilielezwa kuwa Aprili 6, 2026 katika Kijiji cha Mshani, Wilaya ya Sumbawanga, vijana hao walimzushia Issa Athumani Kidungwe (56), mkazi wa Handeni mkoani Tanga, kuwa ameiba nyeti zao, jambo lililosababisha kushambuliwa na wananchi na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili.

Wakati huo huo, watuhumiwa wengine watano bado wanashikiliwa na Polisi, ambao ni Geofrey Milumba Deminic (24), Jafari Nebart Shanjila (25), wakazi wa Kijiji cha Kilangawana, Huruma Geofrey Kasonso (18), mkazi wa Kilyamatundu, pamoja na Costantino Octavian Kiatu (28) na Severino Cosmas Ngonyani (22), wakazi wa Sumbawanga. Taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea kukamilishwa.

Jeshi la Polisi limeonya wananchi kuacha tabia ya kuzusha taharuki zisizo na ukweli, huku likisisitiza umuhimu wa kufuata sheria kwa kutoruhusu mtu yeyote kujichukulia hatua mkononi.

Aidha, wananchi wametakiwa kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya usalama wanapobaini viashiria vya vurugu au uhalifu ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wakati.

Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad