HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 30, 2026

POLISI RUKWA YAWADAKA WATUHUMIWA WA UKATILI DHIDI YA WATOTO

 

JESHI la Polisi Mkoa wa Rukwa limewakamata watu wawili kwa tuhuma za kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto, ikiwemo kuwachoma moto na kuwasababishia majeraha makubwa, katika matukio tofauti yaliyotokea wilayani Kalambo na Sumbawanga.

Watuhumiwa hao ni Fortunatus Benezet Mawela (60), mkazi wa kijiji cha Singiwe, Wilaya ya Kalambo, pamoja na Aisha Credo Mpepo (25), mkazi wa kitongoji cha Kasanzama, mji mdogo wa Laela, Wilaya ya Sumbawanga. Inadaiwa kuwa Aprili 19, 2026, Mawela alimchoma moto mjukuu wake wa kiume mwenye umri wa miaka 16 katika maeneo ya tumbo na mapaja, huku akiwa amemfunga mikono na miguu, akimtuhumu kumuibia ndizi.

Katika tukio jingine lililotokea Aprili 27, 2026, Aisha Credo Mpepo anadaiwa kumuunguza mgongoni mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 8 kwa kutumia pasi ya umeme, akimtuhumu kumuibia shilingi 2,000 zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya kununulia mkaa.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa taratibu zinaendelea kukamilishwa ili watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Wakati huo huo, Mahakama ya Wilaya ya Kalambo imemhukumu Bosco John Fatachi (38), mkazi wa kijiji cha Kambo, kulipa faini ya shilingi 300,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kumfanyia ukatili mtoto wa miaka 8. Mshtakiwa huyo alithibitika kumpiga mtoto huyo kwa waya wa umeme huku akiwa amemfunga mikono na miguu kwa kamba, akimtuhumu kumuibia pipi zenye thamani ya shilingi 200.

Aidha, Mahakama iliyoongozwa na Hakimu Nickson Temu iliamuru mshtakiwa kulipa fidia ya shilingi 500,000 kwa mtoto huyo, ikisisitiza kuwa adhabu hiyo iwe fundisho kwa jamii dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limelaani vikali vitendo hivyo na kutoa wito kwa wazazi na walezi kuacha kutoa adhabu za kikatili, badala yake kuzingatia malezi bora na yenye kuzingatia haki za mtoto. Pia limewapongeza wananchi wanaoendelea kutoa taarifa zinazosaidia kufichua vitendo vya ukatili majumbani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad