HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 30, 2026

FUNGUO Yaendeleza Jitihada za Kukuza Ubunifu Unaoongozwa na Vijana wa Vyuo Vikuu

Mkuu wa Maliasili kupitia Ujumbe wa Umoja wa Ulaya Bw. Lamine Diallo (katikati) akizindua rasmi Wito wa Tano wa Ufadhili wa Kichocheo wa Programu ya FUNGUO Jijini Dar es Salaam.Wengine kutoka kushoto ni Meneja wa Programu ya FUNGUO Bw. Joseph Manirakiza, mwakilishi wa UK FCDO, Bw. Euan Davidson, Mkuu wa Ushirikiano katika Ubalozi wa Finland, Bi. Sana-Liis Taivalmaa na Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP Bw. John Rutere.


· Yazindua Wito wa 5 wa Ufadhili wa Kichocheo

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), kupitia Mpango wa Ubunifu wa FUNGUO, imehitimisha kwa mafanikio Hafla ya Tuzo za #YouthIgnite Awamu ya Tatu na Uzinduzi wa Wito wa 5 wa Ufadhili wa Kichocheo wa FUNGUO, ikiashiria hatua muhimu katika kuimarisha ujasiriamali unaoongozwa na vijana na mifumoya ubunifu katika vyuo vikuu vya Tanzania.

Katika hafla hiyo, FUNGUO ilitunuku biashara 20 zilizoanzishwa na wanafunzi chini ya mpango wa #YouthIgnite Student Founders Fellowship wa awamu ya tatu. Hatua hii inaleta jumla ya biashara zilizoungwa mkono kufikia 60 kupitia awamu tatu, na kuonyesha ukuaji wa mchango wa vyuo vikuu katika uundaji wa ajira na maendeleo ya uchumi.

Meneja wa Mradi wa FUNGUO, Bw Joseph Manirakiza, alitangaza kuongezeka kwa msaada kwa vituo saba vipya vya ubunifu vinavyotegemea vyuo vikuu, na hivyo kufikisha jumla ya vituo vinavyoungwa mkono kote nchini kufikia 17.

“Vituo hivi vina mchango muhimu katika kulea wajasiriamali wachanga kupitia mafunzo, ushauri elekezi, ujasiriamali shirikishi, na upatikanaji wa rasilimali za awali,” alisema.

Hafla hiyo pia ilishuhudia uzinduzi rasmi wa Wito wa 5 wa Ufadhili wa Kichocheo wa FUNGUO, unaolenga biashara bunifu na changa zinazofanya kazi kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, ubunifu wa kidijitali, na madini muhimu—sekta zilizopewa kipaumbele katika maendeleo ya taifa.

Bw. Manirakiza aliendelea kusema kuwa tangu kuanzishwa kwake, FUNGUO imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 7.5 katika biashara changa bunifu (startups) 88 na kusaidia zaidi ya nusu ya biashara hizo kuvutia zaidi ya shilingi bilioni 18 za mitaji ya ziada. Kwa pamoja, biashara hizi zimechangia kuzalisha na kudumisha zaidi ya ajira 10,000 nchini Tanzania.

Mpango wa FUNGUO unatekelezwa na UNDP Tanzania kwa ushirikiano na ANZA Entrepreneurs, kwa msaada wa Umoja wa Ulaya, Serikali ya Finland, na UK FCDO.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania Bw. Jouhn Rutere alisema, “ Kwa kuwekeza katika wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, FUNGUO inasaidia kufanya vyuo vicochee ujasiriamali na kuongeza ajira. Hii inadhihirisha kinachowezekana pale ambapo kuna uwezeshaji kifedha, ushirikiano na ubunifu vinaunganishwa pamoja.”

Naye Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Bw Lamine Diallo alisema EU inajivunia kuiwezesha program ya FUNGUO ambayo inawezesha vijana kubadili mawazo yao ya kibunifu kuwa biashara. “Kufadhili ubunifu unaoongozwa na wanafunzi na sekta nyeti kama kilimo, ubunifu wa kidijitali na madini muhimu kunahitajika ili ukuaji wa uchumi uwe endelevu.

Kwa upande wake, mwakilishi wa UK FCDO, Bw. Euan Davidson naye alisema, kupitia program hii ya FUNGUO, tunashuhudia ni namna gani uwezeshaji wa kifedha unaweza kuchochea uwekezaji binafsi, kukuza ajira na kusaidia biashara ambao zinaashiria dalili njema. Uzinduzi wa Wito wa 5 wa Ufadhili ni hatua muhimu katika kuwezesha ukuaji wa ubunifu Tanzania.”

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad