Ameyasema hayo Aprili 01, 2026 wakati wa kikao kazi cha watumishi wa Bodi kinachoendelea katika Ukumbi wa Chuo Cha Kilimo Sokoine (SUA), mkoani Morogoro, Prof. Msalya alisisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati madhubuti inayotekelezeka kwa vitendo, akieleza kuwa sekta ya maziwa ina nafasi kubwa katika kuboresha lishe, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa taifa.
Alibainisha kuwa ili kufikia malengo ya Bodi, watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano, kuzingatia maadili ya kazi na kuwa wabunifu katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo, hususani katika maeneo ya uzalishaji, ukusanyaji na usindikaji wa maziwa.
“Tunapaswa kuwa chachu ya mabadiliko kwa kuhakikisha kuwa kila hatua tunayochukua inaleta tija kwa wafugaji, wawekezaji na walaji wa maziwa nchini,” alisisitiza Prof. Msalya.
Aidha, alieleza kuwa Bodi itaendelea kuimarisha usimamizi wa ubora wa maziwa pamoja na kurasimisha shughuli za wadau ili kuongeza ushindani wa bidhaa za maziwa za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.
Akizungumza kandokando ya kikao kazi cha watumishi, Mteknolojia wa Chakula Bi. Christabel Swai, alisema kuwa kupitia mijadala na mawazo ya pamoja ya watumishi, Bodi itaweza kubuni mikakati bunifu itakayoboresha utekelezaji wake kwa ufanisi zaidi, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia katika kuleta mageuzi chanya kwenye sekta ya maziwa.
Naye Afisa Masoko Mwandamizi Bw. Hamis Kiimbi, alisema kuwa matarajio ya kikao hicho kitaibua mikakati thabiti ya kukuza masoko ya maziwa na bidhaa zake ndani na nje ya nchi na kuona ongezeko la uelewa kwa walaji kuhusu umuhimu wa matumizi ya maziwa, pamoja na kuimarishwa kwa mifumo ya masoko itakayowawezesha wafugaji na wadau wengine kupata masoko yenye tija zaidi, hivyo kuongeza kipato na kuchochea ukuaji wa sekta ya maziwa nchini.
Kikao kazi hicho cha siku mbili kinalenga kupitia na kujadili Mpango Mkakati wa Bodi wa miaka mitano ijayo, huku kikitarajiwa kutoa mwelekeo mpya wa kuifanya sekta ya maziwa kuwa ya kisasa, yenye tija na inayochangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa.




No comments:
Post a Comment