HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 1, 2026

ELIMU YA MIRATHI YATAJWA SULUHISHO LA MIGOGORO YA URITHI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

CHUO Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam katika kituo chake cha Tegeta, kimetoa elimu ya uelewa kwa wanawake 200 kuhusu usimamizi wa mirathi, ikiwa ni jitihada za kupunguza migogoro ya kifamilia inayotokana na masuala ya urithi.

Akizungumza Aprili 1, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa semina hiyo, Rasi wa Chuo hicho, Prof. Cyricus Binamungu, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mpango endelevu wa kuwakutanisha wanajamii ili kuwajengea uelewa mpana juu ya masuala ya mirathi.

Amesema usimamizi wa mirathi ni suala nyeti, huku mali nyingi zikibaki katika akaunti za mahakama zikisubiri kuchukuliwa na warithi kutokana na migogoro isiyoisha miongoni mwa familia.

“Unakuta mali nyingi zipo mahakamani zinasubiri warithi, lakini migogoro inapochelewesha taratibu, mali hizo haziwafikii walengwa kwa wakati,” amesema Prof. Binamungu.

Ameongeza kuwa wanaamini elimu hiyo itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro hiyo na kuwezesha familia kusimamia vyema urithi wao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tegeta, Bered Ntabaliba, amekipongeza chuo hicho kwa kuwafikishia wananchi elimu hiyo muhimu, akieleza kuwa itawasaidia wanawake kujisimamia na kufuatilia masuala ya mirathi kwa ufanisi zaidi.

Amesema eneo la Tegeta limekuwa likikumbwa na migogoro mingi ya mirathi, hivyo semina hiyo itachangia kupunguza changamoto hiyo kwa kuwapa wananchi uelewa wa sheria na taratibu husika.

“Hili ni somo muhimu sana kwetu, litasaidia wananchi kuelewa namna ya kurithi mali na kuepuka migogoro ya kifamilia,” amesema Ntabaliba.

Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wameishukuru Mzumbe kwa kuwapatia mafunzo hayo, huku wakitoa wito kwa taasisi nyingine kuendelea kutoa elimu kama hiyo ili kupunguza migogoro inayojitokeza katika jamii, hususan ndani ya familia.















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad