HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 13, 2026

DCEA YAKAMATA KILOGRAMU 1983 ZA DAWA ZA KULEVYA, DIWANI NA WENZAKE 77 MBARONI

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata kilogramu 101.2 za dawa za kulevya aina ya mirungi katika eneo la Tabata Kibo jijini Dar es Salaam, zikiwa zimefichwa ndani ya basi la abiria.

Basi hilo aina ya Yutong la kampuni ya Abood, lenye namba ya usajili T 181 EMJ, lilikuwa likifanya safari kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania.

Akizungumza Aprili 14, 2026, Kamishina Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema dawa hizo zilifichwa katika maeneo mbalimbali ya basi hilo, ikiwemo ndani ya mfumo wa hewa (AC), kwa lengo la kukwepa kugundulika.

Alisema watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni dereva wa basi, Ramadhan Mohamed (52), kondakta Salma Sanga (26), pamoja na Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39).

Aidha, katika Mkoa wa Pwani, kilogramu 419.09 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kuelekea Dar es Salaam.

Akifafanua hatua za kisheria, Lyimo alisema kwa mujibu wa sheria, wahusika wanaokamatwa ni wale wanaokutwa na dawa hizo, ambapo katika tukio hilo dereva na kondakta wanashikiliwa pamoja na basi hilo kwa uchunguzi zaidi.

Katika operesheni nyingine zilizofanywa nchini, DCEA imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa mbalimbali za kulevya, kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu, vidonge 286 pamoja na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Sambamba na operesheni hizo, ekari 55.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa na watuhumiwa 77 kukamatwa. Vilevile, magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja vilikamatwa.

Lyimo alisema uchambuzi wa takwimu unaonesha ongezeko la ukamataji wa mirungi, ambapo kilogramu 1,267.12 zilikamatwa, sawa na asilimia 64 ya dawa zote zilizokamatwa katika kipindi husika.

Alieleza kuwa hali hiyo imetokana na mkakati wa mamlaka hiyo kujikita zaidi katika operesheni za dawa za kulevya za mashambani, baada ya kudhibiti kwa kiasi kikubwa mitandao ya dawa za viwandani.

Katika matukio mengine, mkoani Mwanza, kilogramu 52 za mirungi zilikamatwa katika kizuizi cha barabarani cha Magu na Bandari ya Mwanza South, zikiwa zinasafirishwa kwa gari aina ya Fuso (T 296 APA). Dereva wake, Hassan Hassan (37), mkazi wa Mahina Nyamagana alikamatwa.

Wilayani Misungwi, kilogramu 184.9 za mirungi zilikamatwa nyumbani kwa watuhumiwa Chrispin Shoo (62) na mkewe Esther Pastory (55), pamoja na kukamatwa kwa magari mawili aina ya Toyota Crown (T 742 EGL), Toyota Wish (T 854 DXB) na bajaji (MC 261 EZV).

Mkoani Tanga, kilogramu 32.95 za mirungi zilikamatwa zikiwa zimefichwa kwenye mfuko uliochanganywa na maembe, huku mtuhumiwa Seif Omar (38), maarufu kama Haniwao, akikamatwa.

Katika operesheni nyingine mkoani humo, jumla ya kilogramu 164.01 za mirungi zilikamatwa katika matukio tofauti.







No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad