HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 13, 2026

BALOZI OMAR KUONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MIKUTANO YA IMF NA BENKI YA DUNIA

 

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza kikao cha ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings 2026) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), iliyoanza Jijini Washington D.C. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha na Mipango kutoka Ofisi ya Rais-Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali na baadhi ya Taasisi zake.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Washington, D.C)


Na Benny Mwaipaja, Washington D.C,Marekani
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amempongeza Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Balozi Elsie Sia Kanza, kwa kusimamia ipasavyo sera ya Diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na Marekani, ambapo kiwango cha ufanyaji biashara, uwekezaji na utalii kutoka nchi hizo mbili kimeendelea kukua.

Mhe. Balozi Omar ametoa pongezi hizo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani iliyotolewa na Mhe. Balozi Kanza kwa ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), iliyoanza Jijini Washington D.C.

Alisema kuwa ushirikiano wa Tanzania na Marekani umeendelea kuimarika ambapo nchi inatarajia kunufaika zaidi kutokana na mipango thabiti iliyowekwa na ubalozi ambapo miradi mbalimbali katika sekta za biashara, madini na utalii imeongezeka.

“Tunaona uwekezaji mkubwa unakuja kutoka Marekani na huko tunakokwenda tunategemea utakuwa mkubwa zaidi, ikianza kufunguka miradi mitatu minne na mmoja umeutaja upande wa madini ya niobium tunategemea kufanya vizuri zaidi. hatua ya Marriot kuongeza Hoteli kutoka11 kuelekea hoteli 20 ndani ya kipindi cha miaka mitatu inayokuja, maana yake imani ya wenzetu wa Marekani katika Sekta ya utalii inaendelea kuwa kubwa” Alisema Mhe.Balozi Omar.

Akitoa Taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Balozi Kanza alibainisha kuwa thamani ya biashara kati ya nchi hizo imeendelea kukua kwa kasi, ikiongezeka kutoka dola za Marekani 1.15 bilioni mwaka 2023 hadi dola 1.4 bilioni mwaka 2024, sawa na ongezeko la 22.1%. Pia mauzo ya bidhaa za Tanzania Marekani yaliongezeka kwa asilimia 18 mwaka 2025 licha ya changamoto za kimazingira za biashara.

Programu ya AGOA, iliyokuwa imesitishwa tarehe 30 Septemba 2025, imeongezwa muda wa mwaka mmoja hadi 31 Desemba 2026 baada ya kuishawishi nchi hiyo iongeze muda wa kutekeleza program hiyo yenye manufaa makubwa kwa Tanzania ambapo katika miaka ya hivi karibuni mauzo ya nje ya Tanzania Kupitia AGOA yalifikia asilimia 42.85 huku takribani 95% ya mauzo hayo yakihusiana na nguo.

Kwa upande wa uwekezaji, Mhe. Balozi Dkt. Kanza alisema kuwa Kampuni za Marekani zinaendelea kupanua uwekezaji nchini Tanzania ikiwemo Kampuni ya Marriott iliyopanga kuongeza idadi ya hoteli nchini kutoka 11 hadi 20 ifikapo mwaka 2027, na kampuni ya Visa imezindua ofisi ya biashara nchini.

Pia mkataba wa uwekezaji wa dola za Marekani 300 milioni na Panda Hill Tanzania Limited umefadhiliwa na Denham, ukilenga uzalishaji wa madini aina ya niobium mkoani Songwe unaotarajiwa kuzalisha ajira ya watu takriban 600.

“Katika sekta ya utalii, Marekani imeendelea kuwa chanzo kikuu cha watalii na wawindaji wanaoitembelea Tanzania; idadi ya watalii kutoka Marekani iliongezeka kutoka 118,108 mwaka 2023 hadi takriban 145,000 mwaka 2024, huku zaidi ya 60% ya wawindaji wote wakiwa kutoka Marekani. Filamu ya “The Royal Tour” iliyoigizwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ilichangia ongezeko hilo. Alifafanua zaidi Mhe. Balozi Kanza

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha na Mipango kutoka Ofisi ya Rais-Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali na baadhi ya Taasisi zake.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad