HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 30, 2026

Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Mgeni Rasmi wa Tamasha la Pasaka

 

*Tamasha la Pasaka Mtoko na Christina Shusho

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi Aprili 5, 2026 siku ya Jumapili ya Pasaka katika Tamasha la ‘Mtoko na Christina Shusho Pasaka’ ambalo wananchi wataingia bila malipo Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

kauli mbiu katika Mtoko na Christina Shusho ni Ushindi wa Milele.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Machi 30, 2026, Meneja wa msanii wa muziki wa injili Christina Shusho, Humphrey Gatimu amesema maandalizi ya tamasha hilo ambalo linatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Mlimani City yamekamilika na kusisitiza kuwa wananchi wote wanakaribishwa kiushiriki bila malipo yoyote.

Amesema tamasha hilo litawakutanisha waimbaji mbalimbali wa muziki wa injili akiwemo Rose Muhando, Joel Lwaga, The Voice, Bella Kombo, Ambwene Mwasongwe, Neema Gospel Choir, Paul Clement na wengine wengi.

“Milango ya ukumbi itafunguliwa rasmi saa nane mchana, hivyo tunawaomba wananchi kujitokeza kwa wingi na kuwahi mapema ili kuepuka changamoto ya kukosa nafasi ndani,” amesema Gatimu.

Aidha, Gatimu amebainisha kuwa matarajio ya waandaaji ni kupanua wigo wa tamasha hilo mwakani kwa kulipeleka katika mikoa mitatu tofauti, huku wakiahidi kuweka wazi maeneo hayo wakati utakapofika.

Kwa upande wake, mwimbaji wa nyimbo za injili, Shusho amesema tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka kipindi cha Pasaka, limekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wasanii wa muziki wa injili, waumini pamoja na familia kwa lengo la kusherehekea sikukuu hiyo na kuinua vipaji vipya.

Amesema mafanikio ya tamasha hilo yanatokana na amani iliyopo nchini Tanzania, akimshukuru Mungu kwa kumpatia kibali cha kufanya tamasha pamoja na viongozi wa serikali kwa kuendelea kudumisha utulivu na maendeleo ya taifa.

“Tunawahimiza watu kufika mapema ili waweze kushiriki kikamilifu ibada ya sifa na kuabudu pamoja nasi, kwani kuna mambo mengi mazuri yameandaliwa kwa ajili ya kumtukuza Mungu,” amesema Shusho.

Naye mwimbaji kutoka kundi la The Voice, Obedi Mark amesema tamasha hilo limekuwa chachu kwa wasanii wengi kukuza vipaji vyao sambamba na kueneza ujumbe wa injili kupitia muziki.

Kwa upande wake mwanakwaya wa kwaya ya Mt Cecilia Makuburi, Joseph Atanasi amesema wao kama kwaya watashiriki kikamilifu katika tamasha hilo wakiwa wamejiandaa vyema kuendelea kumsifu Mungu kupitia uimbaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad