Dar es Salaam, Tanzania
Zaidi ya wanafunzi 62,000 kote Tanzania sasa wananufaika na majiko salama na safi zaidi kufuatia usakinishaji wa zaidi ya majiko ya kisasa 170 ya nishati safi ya kupikia katika shule na taasisi za umma zaidi ya 45. Hatua hii muhimu iliadhimishwa katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Msingi Bunge jijini Dar es Salaam, ikionesha mchango wa mpango huu katika kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kukabiliana na ukataji wa miti.
Mpango huu unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kupitia programu ya CookFund.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba alisema:
“Mapinduzi haya kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kipaumbele cha kimkakati cha taifa kinachochangia kulinda mazingira, kuboresha afya ya umma na kuongeza ufanisi wa kiuchumi. Kwa kuzipatia shule na taasisi za umma teknolojia za kisasa za kupikia, tunalenga kulinda misitu yetu, kupunguza hewa chafuzi, na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wetu. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kupanua upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034).”
Jitihada za nishati safi ya kupikia nchini zinaongozwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wizara na taasisi nyingine za Serikali, ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, pamoja na taasisi nyingine za umma. Hadi sasa, msaada huu kwa taasisi za umma, hususan shule, unalenga taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa wakati mmoja ili kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Hatua hizi zinaendana na vipaumbele vya kitaifa vya kupunguza ukataji wa miti, kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma. Matumizi ya kuni na mkaa huzalisha chembechembe hatarishi zinazoweza kusababisha magonjwa mbalimbali ya mfumo wa upumuaji kama pumu na saratani ya mapafu.
Kupitia programu ya CookFund, inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya, hatua hizi zinalenga kupunguza matumizi ya nishati za kuni na mkaa kwenda kwenye teknolojia bora na zenye ufanisi zaidi kama majiko yanayotumia mkaa mbadala, majiko ya umeme (electric pressure cookers), biyoethano, majiko banifu, pamoja na gesi. Teknolojia hizi zinatarajiwa kupunguza shinikizo kwa rasilimali za misitu, kuboresha ubora wa hewa jikoni, na kuongeza afya na usalama wa wanafunzi na watumishi. Hadi sasa, taasisi 45 zimeboresha mifumo yao ya upishi, nyingi zikiwa ni shule za msingi na sekondari.
Aidha, kupitia CookFund, UNCDF inatoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa makampuni na wajasiriamali wanaokidhi vigezo ili kuongeza usambazaji wa nishati safi ya kupikia. Msaada huu unajumuisha uwekezaji wa mtaji na mtaji wa uendeshaji kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa biashara zinazojihusisha na uzalishaji, uagizaji, usambazaji na uuzaji wa majiko, mafuta na bidhaa au huduma zinazohusiana na nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Marc Stalmans, alisema:
“Umoja wa Ulaya umejikita kikamilifu katika kuendeleza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani, na Tanzania siyo tofauti. Mpango huu ni sehemu ya juhudi zetu za kusaidia mpito kuelekea nishati safi. Kupitia msaada wa Umoja wa Ulaya, jamii zinazingatia mbinu endelevu zinazolinda mazingira, huku zikichochea ukuaji wa uchumi, kukuza ajira, na kuboresha upatikanaji wa nishati mashuleni, kwenye biashara pamoja na kaya.”
Naye Mshauri Mkuu Maswala Kiufundi wa UNCDF, Bw. Peter Malika, alibainisha kuwa pamoja na msaada uliotolewa kwa taasisi 45 katika wilaya 14 za Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mwanza, programu hiyo imewekeza dola milioni 10.1 katika biashara ndogo na za kati 102.
“Nishati safi ya kupikia inapunguza utegemezi wa kuni na mkaa huku ikiboresha usalama, afya na ufanisi wa majiko shuleni,” alisema Bw. Malika. “CookFund inaonesha wazi kuwa teknolojia za kisasa za nishati zinaweza kuleta mageuzi makubwa katika taasisi za umma na kuboresha moja kwa moja mazingira ya kujifunzia kwa maelfu ya wanafunzi.”
Kwa ujumla, programu hii imeleta matokeo chanya na yenye mageuzi makubwa, ikichangia uundaji wa ajira 27,005 (za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja), jumla ya biashara 4,933 katika mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia, kufikia kaya zaidi ya 482,089, na kupunguza zaidi ya tani 3,911,450 za uzalishaji wa hewa ukaa. Mafanikio haya yanaonesha mchango mkubwa wa programu hii katika maendeleo endelevu, ustawi wa jamii na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania.
Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa UNCDF, Bw. Peter Malika, akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa vya teknolojia ya upishi salama kwa Shule ya Msingi Bunge jijini Dar es Salaam jana. Serikali ya Tanzania, kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Ujumbe wake nchini, na usimamizi wa programu ukifanywa na Mfuko wa Maendeleo wa Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF), inatekeleza Programu ya CookFund ili kuharakisha mpito wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kaya na taasisi za umma, hususan mashuleni. Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba (wa pili kutoka kulia), alikuwa mgeni rasmi.
Mkuu wa Ushirikiano wa Ujumbe wa EU nchini Tanzania, Bw. Marc Stalmans, akihutubia hadhira wakati wa makabidhiano ya vifaa vya teknolojia ya upishi salama kwa Shule ya Msingi Bunge jijini Dar es Salaam jana. Serikali ya Tanzania, kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Ujumbe wake nchini, na usimamizi wa programu ukifanywa na Mfuko wa Maendeleo wa Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF), inatekeleza Programu ya CookFund ili kuharakisha kipindi cha mpito wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kaya na taasisi za umma, hususan shule. Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba (wa tatu kutoka kulia), alikuwa mgeni rasmi.

No comments:
Post a Comment