HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 4, 2026

DCEA Yakamata Tani 9.93 za Dawa za Kulevya, Watuhumiwa 151 Wanaswa

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata jumla ya tani 9.93 za dawa za kulevya za aina mbalimbali, chupa 1,795 za dawa tiba zenye asili ya kulevya na kuteketeza ekari 87.5 za mashamba ya bangi katika operesheni zilizofanyika maeneo mbalimbali nchini.

Katika operesheni hizo, magari sita na pikipiki 29 vilikamatwa huku watuhumiwa 151 wakinaswa wakihusishwa na uhalifu huo.

Akizungumza Machi 4, 2026 jijini Dar es Salaam, Kamishina Jenerali wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo, alisema kwa kushirikiana na maafisa wa forodha wa kituo cha Mutukula, walifanikiwa kukamata dawa tiba zenye asili ya kulevya zilizokuwa zikiingizwa nchini kinyume cha sheria.

Alizitaja dawa hizo kuwa ni Pethidine boksi 105 zenye chupa 1,045, Morphine Sulphate boksi 31 zenye chupa 310 na Fentanyl boksi 44 zenye chupa 440, zilizokamatwa katika basi la abiria la kampuni ya SR Classic lenye usajili namba 5673AB04 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa Kamishina Jenerali Lyimo, basi hilo lilikuwa likifanya safari zake kati ya Uganda, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na dawa hizo zilibainika wakati wa upekuzi katika kituo cha forodha cha Mutukula wakati basi hilo likiingia nchini.

Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni Hassan Omary Mwambashi maarufu Macheni (50), mkazi wa Mbezi Dar es Salaam; Ibrahim Saidi Malindi (36), Mtanzania anayeishi Kampala, Uganda; Yassa Said Hamood (38), mkazi wa Magomeni Dar es Salaam; Hamad Said Hamad (46), mkazi wa Mombo Tanga; Abdul Athuman Khamis (31), mkazi wa Amana Dar es Salaam; Mohamed Abdallah Sako (34), mkazi wa Ilala; na Mwinshaa Mohamed Abdalla (47), mkazi wa Magomeni.

Lyimo alifafanua kuwa Pethidine, Morphine na Fentanyl ni dawa tiba zenye asili ya kulevya zilizo katika kundi la afyuni (opioids) zinazotumika hospitalini kupunguza maumivu makali kwa wagonjwa wa saratani, ajali, wakati wa upasuaji na kwa wagonjwa wa selimundu. Alionya kuwa dawa hizo zikichepushwa zinaweza kusababisha uraibu wa haraka na madhara makubwa ikiwemo kuathiri mfumo wa fahamu, upumuaji na mapigo ya moyo, na hata kusababisha vifo.

Alisema dawa hizo zinadhibitiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95 pamoja na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba ya TMDA Sura ya 219, ambapo muingizaji na msambazaji wa dawa za nakotiki ni Medical Stores Department (MSD) pekee.
 
Skanka, Mirungi na Heroin Zakamatwa

Katika hatua nyingine, Mamlaka hiyo ilikamata kilogramu 81.883 za bangi aina ya skanka kutoka kwa mtuhumiwa Jontwa Samwel Mwaikonyole (43), mkazi wa Gogoni Kibamba, Dar es Salaam. Dawa hizo zilikutwa ndani ya gari aina ya Scania lenye usajili wa Afrika Kusini CAA 129054 pamoja na tela namba CAA 22911 lililokuwa limebeba matunda aina ya apples.

Eneo la Chanika Buyuni, Dar es Salaam, watuhumiwa Masudi Rajabu (38) na Shafii Mohamed (30) walikamatwa wakiwa na kilogramu 488.64 za skanka.

Jijini Mbeya, watuhumiwa sita walikamatwa kwa nyakati tofauti wakisafirisha skanka, akiwemo Lenard Paulo (21) mkazi wa Sirari, Mara aliyekamatwa na kilogramu 46.46. Wengine ni Maria Kandonga (18), Monica Kandonga (41) na Ibrahim Mwakibete (26) wote wakazi wa Mbeya waliokamatwa na kilogramu 9.68; Joseph Mkwala (30) raia wa Malawi aliyekamatwa na kilogramu 4.62; pamoja na Esther Mbise (22) aliyekamatwa na kilogramu 16.1.

Mkoani Arusha, Fatuma Mussa Mohamed (45) maarufu Mama Arapha na Elibaraka Martin Kingu (29) maarufu Baraka walikamatwa wakiwa na bunda 937 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 363.45. Lyimo alimtaja Mama Arapha kuwa ni mhalifu wa muda mrefu aliyekuwa akiendesha mitandao ya usafirishaji wa mirungi.

Aidha, katika operesheni zilizofanyika mikoa ya Tabora, Tanga, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Katavi, Mtwara, Mara, Morogoro, Kigoma, Ruvuma na Kilimanjaro, zilikamatwa tani 5.24 za bangi, tani 4.04 za mirungi na gramu 72 za heroin.

Kamishina Jenerali Lyimo alisema mafanikio hayo yanaonesha jitihada za Serikali katika kupunguza upatikanaji wa dawa za kulevya nchini. Alisisitiza kuwa Mamlaka itaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha dawa hizo hazichepushwi na zinawafikia wagonjwa wanaostahili badala ya kutumiwa na wahalifu.

“Mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja wetu,” alisisitiza.









No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad