HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 23, 2026

TBS YATEKETEZA BIDHAA HAFIFU ZENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 44.9

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati limeteketeza tani 4.5 za bidhaa hafifu na zilizopigwa marufuku zenye thamani ya shilingi milioni 44,911 katika zoezi lililofanyika Februari 21, 2025.

Bidhaa hizo zilijumuisha vipodozi vyenye viambata sumu, vyakula vilivyoisha muda wa matumizi pamoja na nguo za ndani za mitumba ambazo haziruhusiwi kisheria kuingia nchini kutokana na madhara yake kiafya.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kaimu Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania Kanda ya Kati, Sifa Chamgenzi, amesema bidhaa hizo zilikamatwa katika operesheni za ukaguzi zilizofanyika kuanzia Oktoba 2025 hadi Februari 2026 katika mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa.

Amesema endapo bidhaa hizo zingeendelea kuwepo sokoni, zingesababisha athari kubwa kwa afya za watumiaji na kuathiri uchumi wa Taifa.

“Tunawaasa wafanyabiashara kuacha kuuza bidhaa ambazo hazikidhi matakwa ya viwango, vipodozi vilivyozuiliwa pamoja na bidhaa zilizoisha muda wa matumizi. Wakaguzi wetu wapo kazini muda wote na tunaendelea kushirikiana na wananchi na vyombo vingine vya dola kuhakikisha bidhaa zilizopo sokoni zinakidhi viwango,” amesema.

Aidha, Chamgenzi amesisitiza kuwa TBS itaendelea kuimarisha ukaguzi wa bidhaa katika maeneo ya biashara nchini kote. Aliwataka wafanyabiashara kujenga utamaduni wa kukagua ubora wa bidhaa, hususan vyakula na vipodozi, kabla ya kuziuza.

Ameonya kuwa mfanyabiashara yeyote atakayebainika kukiuka sheria na kanuni za viwango, ikiwemo kuuza bidhaa zilizoisha muda wa matumizi au zilizopigwa marufuku, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za TBS kulinda afya za watumiaji na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa au kuingizwa nchini zinazingatia viwango vilivyowekwa.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad