HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 24, 2026

RC MBONI AWATAKA WAFANYABISHARA SHINYANGA KUSHIRIKI ZOEZI LA ELIMU YA KODI MLANGO KWA MLANGO


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amewataka wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kikamilifu kwa maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanaopita katika sehemu zao za biashara kwa lengo la kuwapatia elimu ya kodi na kusikiliza changamoto na maoni yao kwa lengo la kuboresha huduma za TRA.

Mhita ametoa kauli hiyo leo Februari 23, 2026 mkoani Shinyanga mara baada ya kupokea timu maalum ya TRA, ambayo itatoa elimu ya mlango kwa mlango kwa walipa Kodi katika Mkoa wa Kikodi wa Shinyanga.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia wananchi na wafanyabiashara moja kwa moja ili kuwapatia uelewa sahihi wa masuala ya kodi.

Amesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakishindwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kutokana na kukosa uelewa wa kutosha hivyo wafanyabiashara watumie fursa hiyo ili kupata kuelewa mambo mbalimbali ya kodi

“Ndugu zangu wananchi wa Shinyanga, naomba mtumie fursa hii kujitokeza ili mpate uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kulipa kodi. Wapo baadhi ya watu ambao hawajawa mstari wa mbele kuchangia maendeleo kwa sababu ya uelewa mdogo,” amesema Mhita.

Ameeleza kuwa miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo inatokana na mapato ya kodi, akitaja uboreshaji wa miundombinu ya barabara za lami, ujenzi wa shule, pamoja na kuimarishwa kwa huduma za afya hospitalini.

Aidha, amesema ulipaji wa kodi ni kitendo cha uzalendo kwani huchangia moja kwa moja katika kufanikisha maendeleo endelevu ya taifa, huku akisisitiza kuwa kukwepa kulipa kodi ni changamoto inayopaswa kuepukwa.

“Ningependa Mkoa wa Shinyanga uwe wa mfano kwa kuongoza kwa ulipaji kodi wa hiari bila shuruti. Nina imani wananchi wa Shinyanga ni wazalendo na wataendelea kushiriki kikamilifu katika kulipa kodi,” amesema RC Mhita







No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad