Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude amezindua rasmi awamu ya pili ya Bodi ya Rufaa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (Accountants and Auditors Appeals Board – AAAB) katika hafla iliyofanyika kwa lengo la kuimarisha uwazi, uwajibikaji na weledi katika taaluma ya Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo tarehe 18 Februari 2026, CPA Mkude alieleza kuwa bodi hiyo ina jukumu muhimu la kusikiliza na kuamua rufaa zinazowasilishwa na wahasibu na wakaguzi wa hesabu kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma. Alisisitiza kuwa uzinduzi wa awamu hii ya pili unaashiria kuendelea kwa dhamira ya Serikali ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma na kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote zinazohusika.
“Bodi hii ni mhimili muhimu katika kulinda misingi ya haki, uwazi na taaluma bora. Ni matarajio yetu kuwa wajumbe wa awamu hii ya pili watafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya uadilifu na weledi wa hali ya juu,” alisema CPA Mkude.
Aidha, aliwataka wajumbe wa bodi hiyo mpya kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na weledi ili kuendeleza heshima na hadhi ya taaluma ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini, sambamba na kuimarisha imani ya wadau wa sekta ya fedha.
Awamu hii ya pili ya Bodi ya Rufaa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (AAAB) inatarajiwa kuongeza ufanisi katika utatuzi wa rufaa, kuharakisha utoaji wa maamuzi, na kuimarisha zaidi mifumo ya kitaaluma katika kusimamia maadili na viwango vya kazi kwa wahasibu na wakaguzi wa hesabu nchini.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Rufaa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (AAAB) wakati wa uzinduzi uliofanyika katika ukumbi wa hotel ya APC Bunju jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Rufaa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (AAAB) Jaji Mtaafu Sirillius Matupa akizungumza kuhusu kazi zinazofanywa na Bodi hiyo wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo kwa awamu ya Pili.
Mwakilishi wa Msajili wa Bodi ya Rufaa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (AAAB) Gloria Kaaya akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude akikabidi vitendea kazi kwa wajumbe wa Bodi ya Rufaa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (AAAB) wakiongozwa na Mwenyekiti wa AAAB Jaji Mtaafu Sirillius Matupa wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo kwa awamu ya pili.
Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Rufaa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (AAAB) pamoja na watumishi kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Hesabu Tanzania (NBAA) wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude wakati wa uzindui wa Bodi hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Rufaa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (AAAB) Emmy Hudson akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi mara baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya APC Bunju jijini Dar es Salaam.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Rufaa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (AAAB) wakiongozwa na Mwenyekiti wa AAAB Jaji Mtaafu Sirillius Matupa wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo kwa awamu ya pili.



















No comments:
Post a Comment