
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, imezindua Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya katika Mkoa wa Dar es Salaam. Uzinduzi huo umefanyika tarehe 16 Februari, 2026 na kufuatiwa na Kliniki ya Sheria inayoanza tarehe 16 hadi 22 Februari, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Kamati hiyo, Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Dar es Salaam Albert Chalamila, amewataka Mawakili wa Serikali kutoa elimu na ushauri wa kisheria kwa wananchi watakaohudhuria Kliniki ya Sheria kwa kutumia lugha nyepesi itakayoeleweka kwa urahisi na wananchi.
“Katika mkoa huu kuna changamoto nyingi za kisheria kutokana na ukubwa wa mji na mwingiliano wa kibiashara na kijamii, hivyo muwasikilize wananchi na kuwaelimisha kwa lugha nyepesi na rahisi kueleweka.” Amesema Chalamila
Aidha, Chalamila ameeleza kuwa uwepo wa kamati hizo utasaidia kupunguza mashauri au migogoro dhidi ya Serikali, kutoa huduma za ushauri wa kisheria na kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi, kuwawezesha Mawakili wa Serikali kusimamia utawala wa sheria na kupunguza malalamiko ya kisheria kutoka kwa wananchi.
Vilevile Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi katika kliniki hiyo ili waweze kupata huduma za ushauri wa kisheria bure.
“Nitoe wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam mjitokeze kwa wingi kupata huduma hii ya ushauri wa kisheria inayotolewa bure na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.” Amesema Chalamila
Awali, akitoa neno la Utangulizi kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Samwel Maneno amesema kuwa kuzinduliwa kwa Kamati ya Ushauri wa Kisheria na Kliniki ya Sheria katika Mkoa wa Dar es Salaam ni mwendelezo wa juhudi na nia ya dhati za Serikali za kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi.
“Kwa namna ya kipekee niwashukuru sana wananchi waliojitokeza na kuungana nasi katika uzinduzi wa Kamati hii.” Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Sambamba na hilo, Maneno ameeleza kuwa Kliniki ya Sheria iliyozinduliwa itajikita katika kutoa huduma elekezi na wezeshi kwa wananchi, kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi na kushughulikia changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
“Hizi ni Kamati zenu Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya, niwaombe kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itashirikiana pamoja nanyi na naomba mzitumie katika kuwasaidia wananchi kutatua kero zao". Amsema Maneno
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema kuwa kupitia Kamati za Ushauri wa Kisheria zinazoendelea kuzinduliwa katika maeneo mbalimbali nchini Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inategemea kuwafikia wananchi wengi zaidi hususani maeneo ya vijijini.
“Nitoe wito kwa Mawakili wa Serikali kujitoa kwa Weledi katika kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi kwa umahiri mkubwa.” Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Hafla ya Uzinduzi wa Kamati ya Kisheria na Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam imehudhuriwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi, Mkurugenzi Mashtaka, Sylivester Mwakitalu, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Abdul Rajabu Mhinte, pamoja na Wakuu wa Wilaya wa Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam.
.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)
No comments:
Post a Comment