HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, February 7, 2026

FURSA AJIRA QATAR ZAVUTIA VIJANA WENGI

Na. OWM - KAM (DSM)

Mamia ya Vijana kutoka Mikoa mbalimbali nchini wamejitokeza katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kushiriki zoezi la usajili wa madereva wanaotarajia kwenda kufanya kazi nchini Qatar.

Zoezi hili ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Serikali ya kuwaunganisha Watanzania na fursa za Ajira nje ya nchi kupitia mifumo rasmi ili kuhakikisha ulinzi wa haki na usalama wao.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Jane Sorogo, amebainisha kuwa mwitikio umekuwa mkubwa ambapo zaidi ya Vijana 1,700 wamejitokeza kuomba nafasi hizo licha ya mahitaji kuwa ni madereva 1,500 pekee.

Akizungumza wakati wa ziara yake chuoni hapo tarehe 06 Februari 2026, Waziri wa Nchi hiyo Mhe. Clement Sangu, amesema Serikali imeweka mifumo imara ya kisheria inayosimamia Ajira hizo ili kulinda maslahi ya Watanzania.

Waziri Sangu pia amebainisha kuwa tangu mwezi Novemba 2025 hadi Januari 2026, jumla ya Watanzania 2,019 wameunganishwa na fursa za Ajira katika nchi za Saudi Arabia, Qatar, Oman, Falme za Kiarabu na kwingineko.

Aidha, amesema Serikali iko mbioni kusaini hati za makubaliano na nchi nyingine 16 ili kuzidi kutanua wigo wa Ajira kwa vijana.

Mhe. Sangu ametoa wito kwa vijana kuendelea kuchangamkia fursa hizo kupitia njia rasmi za Serikali na kuepuka mawakala wasio rasmi kwa maslahi ya usalama wao na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza kwa niaba ya waombaji, mmoja wa madereva waliojitokeza, Hassan Mohamed, amesema ameamua kufuata utaratibu huo rasmi kwa kuwa unatoa uhakika wa ulinzi wa haki na maslahi yake akiwa ugenini.

Juhudi hizi zinaonyesha dhamira ya Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu katika kutengeneza mifumo inayotoa matumaini na usalama kwa nguvu kazi ya kitanzania inayotafuta fursa nje ya mipaka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad