Dar es Salaam, Februari 20, 2026
KAMPUNI ya Airtel Tanzania imemkabidhi gari jipya aina ya Mazda CX-5 Bw. Shakuu Joshua, dereva taxi mwenye umri wa miaka 31 kutoka Kimara-Temboni, baada ya kuibuka mshindi wa zawadi kuu katika kampeni inayoendelea ya “Mwaka Umenyooka na My Airtel Money App.”
Bwana Joshua ameshinda gari mpya baada ya kununua luku ya umeme yenye thamani ya TZS 1,000 kupitia My Airtel Money App. Baada ya kukamilisha muamala huo, alishiriki katika kipengele cha mchezo wa kusokota (digital spin) ndani ya programu hiyo na baadaye kuthibitishwa kuwa mshindi wa zawadi ya juu kufuatia mchakato rasmi wa uhakiki wa Airtel.
Gari hilo limekabidhiwa rasmi nyumbani kwa familia yake huko Ubungo-Msewe, Dar es Salaam, mbele ya wanafamilia na wawakilishi wa jamii.
Akizungumza wakati wa sherehe za makabidhiano, Bwana Joshua amesema taarifa za ushindi huo awali zilikuja kama mshangao. “Kushinda hii Mazda CX-5 imekuwa mshtuko mkubwa. Uzoefu huu umebadilisha maisha yangu kikweli.
Ninaishukuru sana Airtel kwa fursa hii. Mke wangu amepata mtoto hivi karibuni, hivyo gari hili halitasaidia tu mahitaji ya familia yangu bali pia litafungua fursa mpya kwa kazi yangu na maisha ya baadaye. Hii ni hatua kubwa, na ninahisi nimehamasika kufikia makubwa zaidi nikijua kuwa hatua ndogo kama kutumia Airtel Money, inaweza kuleta zawadi kubwa,” amesema Bwana Shakuu Joshua.
Mama wa mshindi wa gari, Bi. Magreth Mtei, ameelezea shukrani na furaha yake kufuatia makabidhiano hayo.
“Namshukuru Mungu! Nina furaha sana na nimejawa na shukrani. Nilipoambiwa kuwa mwanangu ameshinda kupitia Airtel, kwa kweli kwa mda huo sikuweza kuamini. Nilipoliona gari lenyewe kwa macho yangu leo, ndo nikasema kweli mwanangu ameshinda gari. Naishukuru sana Airtel kwa kuwapa watoto wetu na familia fursa nzuri kama hii,” amesema.
Kwa mujibu wa Airtel Tanzania, kampeni hiyo inawahimiza wateja kufanya miamala kupitia My Airtel Money App, ikiwa ni pamoja na kutuma na kupokea pesa, kulipia bili, kununua muda wa maongezi na kununua luku. Miamala inayokidhi vigezo huingiza wateja moja kwa moja kwenye droo za kampeni na mifumo ya kidijitali ya kutoa zawadi.
Mkurugenzi wa Airtel Money, Andrew Lugamba, amebainisha kuwa kampeni hiyo inaendelea kurekodi ushiriki mkubwa nchi nzima.
“Hadi sasa, kampeni imetoa zaidi ya Bajaj saba, seti za televisheni zaidi ya 30, pikipiki nane, na gari moja la Mazda CX-5. Magari mengine mawili ya Mazda CX-5 yamepangwa kutolewa kabla ya kampeni kuhitimishwa. Lengo letu ni kutoa zawadi kwa uaminifu wa wateja wetu huku tukiimarisha ujumuishaji wa huduma za kifedha kidijitali,” amesema. Airtel Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kupanua ufikiaji wa huduma za kifedha za kidijitali zilizo rahisi na salama kupitia kampeni zinazomlenga mteja na mifumo inayochochewa na teknolojia.

.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment