HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 5, 2026

ADEM, VVOB WAFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KATIKA UONGOZI WA SHULE



Wakala wa Maendeleo ya Usimamizi wa Elimu (ADEM) kwa kushirikiana na VVOB – Education for Development umefikia hatua muhimu katika kuimarisha uongozi wa shule nchini Tanzania kufuatia utekelezaji wenye mafanikio wa Mradi wa LIT-LEAD.

Kupitia mradi huo, timu ya wataalamu wa elimu ilifanya zoezi la kina la ukusanyaji wa takwimu katika mikoa sita ya Tanzania Bara ambayo ni Mbeya, Singida, Katavi, Simiyu, Manyara na Morogoro, kwa lengo la kutathmini hali ya sasa ya uongozi wa shule na kubaini maeneo ya kipaumbele yanayohitaji kuboreshwa.

Mradi huo pia umefanikisha uandaaji wa miongozo ya mafunzo ya vitendo na inayozingatia mazingira halisi ya shule, ambayo sasa iko tayari kutumika katika kuwajengea uwezo wakuu wa shule za sekondari nchini Tanzania Bara. Miongozo hiyo imelenga kuimarisha ujuzi wa uongozi, usimamizi na usimamizi wa ufundishaji (instructional supervision), hatua itakayochangia kuboresha ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Akizungumza katika kikao cha mapitio ya mradi, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, aliusifu ushirikiano imara kati ya ADEM na VVOB, akieleza kuwa ni wa wakati muafaka na wenye matokeo chanya.

“Ushirikiano huu kati ya ADEM na VVOB ni wa kimkakati. Umeweka msingi thabiti utakaoleta mabadiliko chanya na endelevu katika uongozi wa shule, hususan shule za sekondari nchini Tanzania,” alisema Dkt. Maulid.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Programu wa Kimataifa wa VVOB, Bw. Tom Vandenbosch, alieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.

“Tumeridhishwa sana na namna ushirikiano wetu na ADEM unavyoendelea. Kazi ya awali imefanyika kwa umakini mkubwa, na tuna imani kuwa sasa tuko tayari kuanza mafunzo ya wakuu wa shule nchini Tanzania,” alisema.



Mradi wa LIT-LEAD unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uwezo wa uongozi miongoni mwa wakuu wa shule, jambo litakaloboresha usimamizi wa shule na kujenga mazingira bora ya ujifunzaji kwa wanafunzi kote nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad