HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 28, 2026

WANANCHI BAHI YAZINDUA KAMPENI YA UPANDAJI MITI, MITI 20,000 KUPANDA



Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi  Francis Kasambala akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti ngazi ya Jamii leo Januari 28,2026 huko Bahi Mkoani Dodoma, mwenye T-shirt nyeusi ni Mku wa Idara ya Mafunzo wa INADES-Formation Tanzania Michael Kihwele. Katika kampeni hiyo, jumla ya miti 2000 kati ya 6000 imepandwa ambapo jumla ya miche 20,000 inatarajiwa kupandwa katika vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo.





Na Mwandishi Wetu Michuzi TV, Dodoma.
KATIKA kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za utunzaji wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, wananchi wa Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma wamezindua kampeni ya upandaji miti ngazi ya jamii, ambapo jumla ya miche 20,000 inatarajiwa kupandwa katika vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo.

Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo Januari 28, 2029 katika Shule ya Sekondari Mchingu iliyopo Bahi, ambapo wananchi kutoka vijiji vya Mndemu, Kisima cha Ndege, Chilungilu na Mkondai kwa pamoja walipanda miche 2,000 kati ya jumla ya miti 6,000 inayotarajiwa kupandwa katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Francis Kasambala, aliyemwakilisha Mgeni Rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kuchukua hatua za vitendo katika uhifadhi wa mazingira.

Alisema kampeni hiyo ni kielelezo cha mshikamano wa jamii katika kulinda rasilimali za asili na kuongeza ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kasambala alisisitiza kuwa upandaji miti si tukio la siku moja, bali ni mchakato unaohitaji uangalizi na uwajibikaji wa pamoja ili kuhakikisha miche yote inakua na kuleta tija kwa jamii, ikiwemo kuboresha rutuba ya udongo, kuhifadhi vyanzo vya maji na kuimarisha usalama wa chakula.

Akizungumza kwa niaba ya Shirika la INADES-Formation Tanzania, Mkuu wa Idara ya Mafunzo, Michael Kihwele, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa shirika hilo, Jacqueline Nicodemus, alisema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa miaka mitatu unaofadhiliwa na shirika la Bread for the World.

Mradi huo unalenga kuwawezesha wanajamii wa vijijini katika Halmashauri za Bahi, Chemba na Kondoa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Aliongeza kuwa kupitia kampeni hiyo, jamii itaendelea kupata elimu ya mazingira, mafunzo ya vitendo na ushirikiano wa karibu na Serikali za Mitaa pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), huku shughuli za upandaji na ufuatiliaji wa miti zikiendelea hadi msimu wa mvua utakapokamilika.

Kampeni hiyo inaendeshwa chini ya kaulimbiu isemayo “Panda Mti, Tuilinde Kesho”, ikilenga kuhamasisha jamii kuchukua jukumu la kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad