Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imezindua siku ya Taaluma ya Uhasibu "Annual Accountancy Career Day" yenye lengo la kuimarisha na kukuza taaluma ya uhasibu nchini. Sambamba na hilo Bodi imefanya uzinduzi wa mfumo utakaowakutanisha pamoja waajiri, wanachama wa Uhasibu, Wanafunzi wa Vyuo mbalimbali kutoka (CBE, UDSM, NIT, IFM, TIA, Mzumbe, Chuo cha Kodi, Chuo Kikuu cha Ardhi nk.) pamoja na wanazuoni "NBAA Accountancy Hub".
Akifungua jukwaa hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, CPA. Prof. Sylvia S. Temu, amesema kuwa wazo la kuandaa siku hiyo ya Taaluma ya Uhasibu "Annual Accountancy Career Day" lilitokana na jitihada za makusudi za Bodi kutafuta siku maalum ya kuwakutanisha wanafunzi wa Elimu ya juu, watahiniwa wa mitihani ya Bodi na waajiri ili wakae pamoja na kujadiliana mustakabali wa taaluma ya Uhasibu nchini.
CPA. Prof. Temu alisema Bodi inatarajia jukwaa hilo kuleta matokeo makubwa, akibainisha kuwa ni fursa ya kipekee inayokutanisha kizazi kipya cha wahasibu na wahasibu wabobezi pamoja na waajiri kutoka sekta mbalimbali. Alieleza kuwa jukwaa hilo linaweka mazingira bora ya kuchagiza maono, matarajio na matumaini ya wahasibu wa sasa na wa baadaye.
Aliongeza kuwa NBAA inapenda kusikia moja kwa moja mawazo, matarajio na changamoto zinazowakabili wanafunzi na watahiniwa wa Mitihani ya Bodi katika safari yao ya kitaaluma, ili Bodi na wadau wake waendelee kuijenga taaluma ya Uhasibu kwa kuzingatia uhalisia wa mazingira ya kazi.
Aidha, alisema jukwaa hilo linawakutanisha washiriki na taasisi za sekta binafsi na za umma, jambo linalowapa fursa ya kupata uzoefu na kuwaunganisha moja kwa moja na wahasibu wabobezi pamoja na waajiri, ili kuelewa mahitaji halisi ya soko la ajira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno, alisema kuwa "Annual Accountancy Career Day" ni nguzo muhimu katika maandalizi ya watahiniwa wa Mitihani ya Bodi na maisha ya kazi, kwa kujenga daraja kati ya elimu ya kitaaluma darasani na uhalisia wa taaluma ya Uhasibu.
Katika jukwaa hilo, kulikuwa na mabanda takribani 30 kutoka kwa waajiri na taasisi mbalimbali, zikiwemo Taasisi za Serikali, Taasisi za fedha, kampuni za Ukaguzi na Uhasibu, ambapo washiriki walipata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na waajiri.
Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, CPA. Prof. Sylvia S. Temu akisoma hotuba ya ufunguzi wa siku ya Taaluma ya Uhasibu "Annual Accountancy Career Day" yenye lengo la kuimarisha na kukuza taaluma ya uhasibu nchini. Sambamba na hilo Bodi imefanya uzinduzi wa mfumo utakaowakutanisha pamoja waajiri, wanachama wa Uhasibu, Wanafunzi wa Vyuo pamoja na wanazuoni "NBAA Accountancy Hub". uliofanyika katika ofisi za NBAA jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno akizungumza kuhusu mchakato wa kuanzisha "Annual Accountancy Career Day" ili kuwakutanisha waajiri, wanachama wa Uhasibu na Ukaguzi, Wanafunzi wa Vyuo pamoja na wanazuoni ili kuendeleza taaluma ya Uhasibu nchini.
Mkurugenzi wa Huduma za Shirika kutoka NBAA CPA Kulwa Malendeja akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa "Annual Accountancy Career Day" uliofanyika katika ofisi za NBAA jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali (CBE, UDSM, NIT, IFM, TIA, Mzumbe, Chuo cha Kodi, Chuo Kikuu cha Ardhi nk.) pamoja na wadau wa Uhasibu wakifuatilia hotuba za ufunguzi wa "Annual Accountancy Career Day" uliofanyika katika ofisi za NBAA jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, CPA. Prof. Sylvia S. Temu akikabidhi vyeti pamoja na tuzo kwa kutambua mchango wa wadhamini wa "Annual Accountancy Career Day" iliyofanyika katika ofisi za NBAA, Mhasibu House jijini Dar es Salaam tarehe 13/01/2026.
Picha za pamoja za meza kuu, waajiri, wadhamini na washiriki wa siku ya taaluma ya Uhasibu




























No comments:
Post a Comment