TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), inahitaji shilingi bilioni 1.6 kwaajili ya kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto 420 wanaougua maradhi ya moyo ambao wazazi wao hawana uwezo wa kugharamia matibabu yao.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Taasisi ya Heart Team Foundation Africa, Dk Naiz Majani, aliyezungumza kwa niaba ya JKCI wakati wa hafa ya kuupongeza mgodi wa madini wa Geita Gold Mine (GGM) kwa kusaidia upasuaji wa watoto 14 wanaougua moyo katika taasisi hiyo.
Alisema HTFA kwa kushirikiana na JKCI mwaka jana walifanya harambee kukusanya fedha za matibabu kwa wagonjwa wa moyo ambapo GGM ni miongoni mwa wadau wengi waliotoa fedha kugharamia matibabu hayo.
“Tulipowaomba GGM walichangia shilingi milioni 56, matibabu ya moyo ni gharama kubwa sana duniani kote na kwa hapa Tanzania asilimia 70 ya matibabu hayo gharama inakuwa kwa serikali na asilimia 30 kwa wazazi lakini bado asilimia 30 ni kubwa sana kwa mtanzania wa kawaida,” alisema
Alisema kwa mwaka 2025 HTAF ilifanikiwa kusaidia watoto 303 kupata matibabu ya moyo kwa upasuaji wa moyo na asilimia tano wamesaidiwa na GGM na maendeleo yao ni mazuri kwa kiwango cha asilimia 95.
Alisema watoto waliosaidiwa na kufanyiwa upasuaji kupitia fedha zilizotolewa na GGM wametoka mikoa 11 ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Iringa, Lindi, Kibosho, Mbeya, Singida, Handeni, Pwani na Mbeya.
Dk Naiz alisema katika kila watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai mmoja au wawili wanakuwa na tatizo la moyo na kuongeza kuwa takwimu za hapa nchini ni kwamba kila mwaka wanazaliwa watoto milioni mbili kwa hiyo kuna watoto 10,000 ambao kila mwaka wanazaliwa na matatizo ya moyo.
Makamu wa Rais wa GGM, Simon Shayo, alisema wanaona fahari kuwa sehemu ya jitihada za kusaidia kuokoa maisha ya watoto wanaougua moyo na alitoa wito kwa taasisi mbalimbali kuunga mkono jitihada zinazofanywa na JKCI kuokoa maisha ya watoto wanaougua moyo.
“GGM tunajisikia fahari kubwa sana kuwa sehemu ya juhudi hizi, hatujutii na tunaona ni wajibu wetu kuwasaidia watanzania katika sekta hii ya afya, napenda kuwaambia watu wa sekta binafsi kuwa biashara unayofanya itakuwa na faida tu pale itakapokuwa inasaidia kubadilisha ustawi wa watu,” alisema
“Hapa JKCI kuna kazi ya kuwaokoa watoto na kurejesha tabasamu kwao, sisi GGM tunaahidi kuendelea kushirikiana na JKCI, ingawa hatujapata maombi rasmi lakini naamini mkileta ombi tutaweka kwenye mpango wetu wa utekelezaji,” alisema
Mkurugenzi Mkuu wa Global Medicare, Abdulmalik Mollel aliishukuru GGM kwa namna ambavyo imekuwa mstari wa mbele kusaidia watoto wanaougua moyo kutibiwa katika taasisi ya JKCI.







No comments:
Post a Comment