Mkutano wa 18 wa pamoja wa mapitio ya Sekta ya Usafirishaji(JTSR) umeendelea siku ya pili tarehe 16 Desemba, 2025 katika ukumbi wa AICC Jijini Arusha, ukiongozwa na katibu mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof.Godius Kahyarara
Wakuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Majini (TASAC) wameeleza hatua zilizofikiwa katika kuimarisha mifumo ya udhibiti, usalama na ufanisi wa huduma za usafiri, huku wakibainisha mikakati ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya teknolojia na ongezeko la mahitaji ya usafiri.
Kwa upande wa TPA, imewasilisha mada kuhusu maboresho ya miundombinu ya bandari, ongezeko la ufanisi wa kuhudumia mizigo na mchango wa bandari katika kukuza biashara ya kikanda na kimataifa huku TASHICO ikielezea mipango ya ujenzi wa Meli mpya na uboreshaji wa meli zilizopo katika kuongeza ufanisi.
Shirika la Reli Tanzania (TRC) na TAZARA zilielezea maendeleo ya miradi ya reli ikiwemo reli ya kisasa ya SGR na MGR, maboresho ya reli ya TAZARA na michango yake katika kupunguza gharama za usafirishaji na kuimarisha muunganiko wa kikanda.
Chuo cha Usimamizi wa Bandari (Bandari College), NIT na DMI vimewasilisha mada zinazohusu maendeleo ya rasilimali watu, mafunzo ya kitaalamu na maandalizi ya wataalam wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya sekta ya usafirishaji.
Aidha, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeeleza mchango wa taarifa za hali ya hewa katika kuhakikisha usalama wa usafiri wa anga, majini na ardhini, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ilibainisha mikakati ya kuboresha ufanisi wa uendeshaji, upanuzi wa mtandao wa safari na mchango wake katika kukuza utalii na biashara huku,TAA ikielezea ujenzi na maboresho ya Viwanja vya ndege nchini.
Kwa ujumla, siku ya pili ya mkutano imejikita katika tathmini ya kina ya utendaji wa taasisi, kubadilishana uzoefu na kuainisha maeneo yanayohitaji maboresho ili kuhakikisha sekta ya usafirishaji inakuwa jumuishi, shindani na endelevu, Mkutano huo unatarajiwa kufungwa rasmi Tarehe 17 Desemba, 2025 na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa


.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment