Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imewakumbusha watumiaji wa droni maarufu kama ndege nyuki kuzingatia sheria na kanuni za usalama wa usafiri wa anga nchini, wakati wa matumizi ya teknolojia hiyo inayokua kwa kasi nchini na duniani kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi, amesema kuwa teknolojia ya droni ni miongoni mwa bunifu muhimu zilizoleta manufaa makubwa kwa jamii za Tanzania na duniani kwa ujumla. Ameeleza kuwa teknolojia hiyo iliingia nchini takribani miaka 20 iliyopita na imekuwa ikifanya vizuri na kuleta mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo kilimo, utafiti, ulinzi, upigaji picha na utoaji wa huduma za kijamii.
Msangi amesema kuwa kama ilivyo kwa teknolojia nyingine, teknolojia ya droni "ndege nyuki" ina faida na madhara pia endapo haitasimamiwa na kudhibitiwa vizuri. Amesisitiza kuwa moja ya majukumu ya msingi ya TCAA ni kuhakikisha usalama unapatikana kwa watumiaji wote wa anga la Tanzania.
“Ndugu wanahabari, anga letu ni hazina kubwa sana kwa nchi yetu na ni jukumu la kila mtumiaji kuhakikisha anafuata sheria na kanuni ili anga letu liendelee kuwa salama,” amesema Msangi.
Ameongeza kuwa TCAA inapenda kuwakumbusha wamiliki, watumiaji na waagizaji wote wa droni nchini kwamba matumizi ya droni ni lazima yaambatane na ufuataji wa sheria na taratibu za matumizi sahihi. Kila mmiliki na mtumiaji wa droni, awe ni mfanyabiashara, kampuni, taasisi au mtu binafsi, anatakiwa kuhakikisha kuwa droni yake imesajiliwa, amepata mafunzo na vibali vya matumizi kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania.
Aidha, Msangi amesema kuwa kwa wageni wanaotembelea Tanzania na kutamani kutumia droni zao wakiwa nchini, wanaruhusiwa kufanya hivyo kwa kufuata utaratibu maalum uliowekwa na Mamlaka ambazo zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya TCAA pamoja na mitandao yake ya kijamii.
Kwa upande wa elimu kwa umma, amesema TCAA inaendelea kutoa elimu mara kwa mara kupitia vyombo mbalimbali vya habari, mitandao ya kijamii, makongamano na warsha, ili kuwafikia Watanzania walioamua kujikita katika matumizi ya teknolojia ya droni.
Amehitimisha kwa kuwakumbusha vijana wa Kitanzania kufuata sheria za matumizi sahihi ya droni ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wengine wa anga na kusisitiza kuwa kushindwa kufuata sheria hizo ni kinyume cha sheria za nchi na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matumizi ya droni maarufu kama ndege nyuki na kutoa rai kwa watumiaji kuzingatia sheria na kanuni za usalama wa usafiri wa anga nchini.



No comments:
Post a Comment