Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Temeke umebaini vitendo vya udanganyifu katika baadhi ya mabucha yanayouza nyama, baada ya kufanya operesheni maalum ya ukaguzi wa mizani inayotumika kuuzia wananchi.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Meneja wa Wakala wa Vipimo
Mkoa wa Temeke, Elolymus Hilary Maunde, amesema operesheni hiyo ilifanyika
mwishoni mwa wiki katika maeneo ya Temeke na Kigamboni, ikiwa na lengo la
kumlinda mlaji dhidi ya udanganyifu unaoweza kumsababishia hasara ya kifedha.
Amesema ukaguzi huo umefanyika katika kipindi hiki cha
kuelekea msimu wa sikukuu ambapo mahitaji ya vitoweo, hususan nyama, huongezeka
kwa kasi, hali inayoweza kuwafanya baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu
kutumia mianya kujinufaisha.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, jumla ya mabucha 17 yalikaguliwa
katika operesheni hiyo, ambapo mabucha matatu yalibainika kuchezea mizani kwa
makusudi ili kuwaibia wananchi. Wamiliki wa mabucha hayo walikamatwa na
kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutozwa faini kwa mujibu wa sheria.
Bwana Maunde amewataka wamiliki wa mabucha kuhakikisha
wanasimamia kwa karibu shughuli za wafanyakazi wao na kutumia mizani
iliyothibitishwa na Wakala wa Vipimo, ili kuepuka adhabu na kulinda uaminifu wa
wateja wao.
Aidha, amewahimiza wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa
zinazopimwa kwa mizani, na kutoa taarifa mapema kwa Wakala wa Vipimo endapo
watabaini viashiria vya udanganyifu. Ofisi za Wakala huo zinapatikana katika
kila mkoa na wilaya nchini kwa ajili ya kupokea malalamiko na kutoa msaada.
Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki
katika zoezi hilo, akiwemo Jumamosi Kenneth Matanira na Joni Nzenze,
wameipongeza Wakala wa Vipimo kwa kufanya operesheni hiyo pamoja na kutoa elimu
kwa wauzaji, wakisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uaminifu kati ya wauzaji na
wateja pamoja na kuboresha biashara zao.
Operesheni hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali
kuhakikisha haki ya mlaji inalindwa na kwamba wananchi wanapata bidhaa kulingana
na thamani halisi ya fedha wanazolipa.

No comments:
Post a Comment