
TANZANIA imeanza hatua mpya katika safari yake ya mageuzi ya kidijitali baada ya ujumbe wa pamoja kati ya Serikali na Asasi za Kiraia kuanza ziara ya kitaalamu nchini Marekani kwa ajili ya kubadilishana uzoefu juu ya usimamizi na uongozi wa mifumo ya kidijitali. Ziara hiyo inaongozwa na Tech & Media Convergency (TMC) chini ya mpango mpana wa Tanzania Digital Collaboration Program, unaofadhiliwa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Bureau of African Affairs ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Ujumbe huo unashiriki katika majadiliano ya ngazi ya juu na taasisi mbalimbali za kimataifa zikiwemo World Bank, Google, National Democratic Institute (NDI) pamoja na wataalamu wa sera za teknolojia, ambapo mazungumzo yanajikita katika mwenendo wa kimataifa, mifumo bora, na masomo yanayoweza kutumika katika mazingira ya Tanzania.
Kupitia ziara hii Tanzania inalenga kuimarisha uwezo wake katika maeneo kadhaa muhimu ya teknolojia na sera, ikiwemo usimamizi wa Internet na mifumo ya udhibiti,Ulinzi mtandao na uthabiti wa mifumo ya taifa,Usimamizi wa takwimu na matumizi salama ya teknolojia,Utoaji wa huduma za umma kwa njia ya kidijitali,Ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa kimataifa
Ziara hii inaakisi mwamko mpana wa umuhimu wa ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuweka msingi imara wa mustakabali wa kidijitali nchini.
Moja ya vipengele vinavyofanya ziara hii kuwa ya kipekee ni kuwaleta pamoja serikali na asasi za kiraia ndani ya ujumbe mmoja rasmi jambo linalolenga kujenga uaminifu, uratibu na mtazamo wa pamoja katika mageuzi ya kidijitali.
Akizungumzia ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TMC, Asha D. Abinallah, alisema “Ziara hii imefungua nafasi adimu na muhimu kwa serikali na asasi za kiraia kujifunza kwa pamoja kutoka kwa viongozi wa kimataifa wa utawala wa kidijitali. Tumejidhatiti kuhakikisha kwamba mageuzi ya kidijitali Tanzania yanakuwa salama, jumuishi na yanayofuata viwango bora vya kimataifa.”
Kwa mujibu wa waandaaji, ziara hii inalenga kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa taifa, ikiwemo kuimarika kwa uwezo wa kutunga sera za kidijitali kwa kuzingatia ushahidi na haki za kidijitali,Ushirikiano bora kati ya Serikali na Asasi za Kiraia,Maarifa ya namna ya kubadilisha mifano ya kimataifa ili ifae mazingira ya Tanzania,Mapendekezo ya kisera kuhusu usalama mtandao, takwimu, teknolojia salama, na ubunifu katika utoaji wa huduma za serikali, Ushirikiano mpya wa kimkakati na taasisi za Marekani kwa ajili ya mageuzi ya muda mrefu
Ziara hii inachukuliwa kuwa hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea kujenga uchumi shindani wa kidijitali, hususan wakati ambapo dunia inaongezeka kutegemea mifumo ya mtandao katika kutoa huduma, uongozi na demokrasia.


No comments:
Post a Comment