Akizungumza katika mkutano huo uliohusisha wadau mbalimbali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, David Ndibalema, alisema shirika hilo limeandaa mafunzo hayo ili kujenga uelewa wa pamoja kwa wazalishaji na waagizaji wa vifaa vya umeme kuhusu viwango vinavyohitajika kwa bidhaa zinazotoka ndani na nje ya nchi.
“Tunakiwango maalumu kwa bidhaa mbalimbali za umeme. Kama mtu anaingiza soketi au waya, lazima akidhi kiwango husika. Tunawapa taratibu za kufuata ili kuhakikisha bidhaa zinazotoka nje zimekaguliwa na kupata cheti cha ubora kabla ya kuingizwa nchini,” amesema Ndibalema.
Ameonya kuwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa ambazo hazijakidhi viwango wanaweza kujikuta wakipata hasara, kwani bidhaa hizo huteketezwa kulingana na kanuni na sheria za viwango.
“Hatupendi kufikia hatua ya kuteketeza bidhaa, lakini tukibaini hazijakidhi viwango, sheria inatamka hivyo. Pia kuna faini kwa atakayekiuka taratibu hizo,” aliongeza.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Mashariki, Noor Meghji, amesema mkutano huo umetoa fursa kwa wafanyabiashara kupata ufafanuzi kuhusu taarifa za ukaguzi na hatua wanazotakiwa kuchukua ili kuhakikisha bidhaa wanazoleta zina ubora unaotakiwa.
“Tumeainisha changamoto mbalimbali na kutoa mwongozo wa nini kinatakiwa kufanyika ili kuimarisha ubora wa bidhaa za umeme zinazoingia sokoni,” amesema.
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, Mhandisi Gilbert Mauto, ambaye ni mzalishaji wa vifaa vya umeme nchini, alisema mafunzo hayo yametolewa kwa wakati na yatawasaidia watengenezaji kuzalisha bidhaa bora zinazoendana na mahitaji ya soko na viwango vya TBS.
Naye msambazaji wa vifaa vya umeme katika soko la Kariakoo, Neema Kiboha, ameipongeza TBS kwa kutoa elimu hiyo, akisema itawasaidia wafanyabiashara kufanya maamuzi sahihi na kuzuia uingizaji wa bidhaa hafifu.
“Ninaahidi kuifikisha elimu hii kwa wateja wangu na wafanyabiashara wenzangu ili kuhakikisha tunalinda soko letu dhidi ya bidhaa zisizofaa,” amesema.




























No comments:
Post a Comment