Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Profesa Peter Msoffe, akizungumza jijini Dar es Salaam leo Desemba 17, 2025 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa majadiliano yatokanayo na mkutano wa mkuu wa mwaka wa 30 wa mabadiliko ya tabianchi.
*Afrika Yapata Mafanikio Makubwa Kwenye Majadiliano ya Mabadiliko ya Tabianchi Brazil
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
NAIBU Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Profesa Peter Msoffe, amesema Tanzania imefanikiwa kupata ahadi za ufadhili wa zaidi ya dola za Kimarekani milioni 440 pamoja na euro 500,000 baada ya kushiriki Mkutano wa 30 wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika jijini Belem, Brazil, huku ikiendelea kuimarisha biashara ya hewa ukaa (carbon) nchini.
Hayo ameyasema leo Desema 17, 2025 wakati akimwakilisha Katibu mkuu, ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Injinia Cpriyan Luhemeja jijini Dar es Salaam katika majadiliano ya baada ya mkutano wa COP30 uliofanyika nchini Brazil.
Prof. Msoffe amesema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo wa kila mwaka umekuwa na umuhimu mkubwa katika kuwasilisha nafasi na msimamo wa nchi kwenye masuala ya mabadiliko ya tabianchi, hususan katika eneo la uhimilivu.
Ameeleza kuwa mwaka huu Tanzania ilishiriki ikiwa pia Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Wataalamu wa Afrika, hali iliyoipa nchi fursa ya kuzungumza kwa niaba ya bara na kushiriki moja kwa moja katika maamuzi ya kimkakati.
Amefafanua kuwa lengo kuu la ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo lilikuwa ni kujadili fursa zitakazosaidia wananchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi mbalimbali inayoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Prof. Msoffe amesema serikali imetoa maelekezo kwa wizara, taasisi za umma na sekta binafsi kuhakikisha bajeti za mazingira zinaelekezwa katika utekelezaji wa mipango inayolingana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo mazingira na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa nguzo kuu.
Ameongeza kuwa taasisi za utafiti, sekta binafsi, taasisi za kifedha pamoja na asasi za kiraia zinaendelea kufanya kazi kwa kuzingatia mwelekeo na maelekezo ya serikali, huku Ofisi ya Makamu wa Rais ikiratibu shughuli hizo ili kuhakikisha hakuna mwingiliano wa majukumu na rasilimali zinatumika kwa ufanisi zaidi.
Akizungumzia ahadi za kifedha zilizopatikana Brazil, Prof. Msoffe amesema hatua inayofuata ni kuzifuatilia kwa karibu ili zigeuke kuwa fedha halisi zitakazosaidia utekelezaji wa miradi ya mazingira nchini. Ameeleza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau wengine itaendelea kuhakikisha ahadi hizo zinatekelezwa kikamilifu.
Kuhusu biashara ya hewa ukaa, Prof. Msoffe amekiri kuwa Tanzania bado ipo nyuma lakini imepiga hatua kubwa kwa kupitisha sheria ya kuanzisha Kituo cha Usimamizi wa Carbon, ambacho tayari kimeanza kazi Morogoro ndani ya Chuo Kikuu cha Sokoine.
Ameeleza kuwa hadi sasa kuna miradi 82 ya carbon iliyo katika hatua mbalimbali, huku maelekezo yakitolewa kuhakikisha miradi hiyo inaanza kuingiza mapato kwa taifa.
Amehitimisha kwa kusema serikali itaendelea kushirikisha wadau muhimu ikiwemo sekta ya fedha, viwanda na makampuni, kuanzia Januari, ili kufungua fursa zaidi katika biashara ya carbon, akisisitiza kuwa biashara hiyo ni kipaumbele cha serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa makundi ya majadiliano ya Afrika na mshauri wa Rais wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi, Dkt. Richard Mayungi, amesema Mkutano wa 30 wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Brazil ulikuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla, kutokana na maamuzi ya kimkakati yaliyolenga fedha, uhimilivu na ustawi wa wananchi wa kawaida.
Dkt. Mayungi amesema mkutano huo uligawanyika katika ajenda mbili kuu, ikiwemo ajenda rasmi chini ya Umoja wa Mataifa na majadiliano ya kuendeleza makubaliano yaliyokuwepo awali. Katika eneo hilo, Afrika ilisisitiza haki ya kupata rasilimali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi bila mzigo wa mikopo, ikizingatiwa kuwa athari hizo zimesababishwa zaidi na nchi zilizoendelea.
Ameeleza kuwa mafanikio makubwa yalipatikana baada ya kukubaliana fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zitolewe kwa mfumo wa ruzuku badala ya mikopo, pamoja na kuimarishwa kwa mifuko ya kimataifa ikiwemo Green Climate Fund, Adaptation Fund, LDC Fund na Loss and Damage Fund, ambapo tayari mfuko huo wa hasara na uharibifu umefikia zaidi ya dola milioni 800.
Kwa upande wa uhimilivu, Dkt.Mayungi amesema mkutano ulipitisha viashiria vya kimataifa vya kupima namna nchi zinavyokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan kwa jamii za vijijini. Ameongeza kuwa nchi zote zitatakiwa ndani ya miaka miwili kuwasilisha taarifa za changamoto, hatua zilizochukuliwa na mahitaji ya msaada kupitia mfumo wa Global Vulnerability Indicators.
Akizungumzia manufaa ya moja kwa moja kwa Tanzania, Dkt. Mayungi amesema nchi imefanikiwa kupewa nafasi ya kuanzisha Kituo cha Vijana cha Afrika kwa ajili ya mafunzo ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na ofisi ya uratibu wa masuala ya majanga yanayotokana na tabianchi chini ya Umoja wa Mataifa. Amehitimisha kwa kusema mafanikio hayo ni matokeo ya uongozi thabiti na ushiriki mzuri wa Tanzania katika majadiliano ya kimataifa.
Matukio mbalimbali wakati wa majadiliano ya baada ya mkutoano wa 30 wa mabadiliko tabianchi uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Desemba 17, 2025.


.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)

No comments:
Post a Comment