
BANJUL, Gambia — Mazungumzo ya kina kati ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo na Dk. Anders Pedersen, mtaalamu maarufu wa jenetiki ya miti na mmoja wa waanzilishi wa Tanzania Tree Seed Agency (TTSA), yamekuwa miongoni mwa matukio muhimu katika siku ya tatu ya kikao cha 25 cha African Forestry and Wildlife Commission (AFWC25), kilichoendelea leo, Desemba 3, 2025 jijini Banjul.
Wawili hao walikutana kando ya kikao na kujadili mustakabali wa upatikanaji wa mbegu bora za miti ikiwa ni nyenzo muhimu katika juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha misitu ya kibiashara na kuongeza uzalishaji wa malighafi za viwanda.
Akizungumzia safari ya taasisi hiyo, Prof. Silayo alisema TTSA iliyoasisiwa miaka ya 1990 ikijengwa juu ya tafiti na ushauri wa wataalamu kama Dkt. Anders, sasa imeimarishwa zaidi kupitia Kitengo cha Uzalishaji Mbegu za Miti ndani ya TFS, ambacho kinahakikisha upatikanaji wa mbegu zilizothibitishwa kisayansi kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi.
“Mbegu bora ndiyo msingi wa misitu imara. Bila chanzo cha kuaminika, hatuwezi kuunda misitu inayostahimili tabianchi na magonjwa. Misitu ya kesho inaanza na mbegu nzuri leo, na mbegu hizo zinapatikana TFS, karibuni,” alisema Prof. Silayo akiwahimiza wadau na wawekezaji kununua mbegu za ubora wa juu kutoka TFS.
Dk. Anders, ambaye amekuwa mshauri wa muda mrefu katika sekta ya mbegu Tanzania na Afrika Mashariki, alisema bara la Afrika liko kwenye nafasi adhimu ya kuongoza dunia katika mageuzi ya misitu endapo litawekeza kikamilifu kwenye ubunifu wa kielimu na vyanzo vya mbegu vilivyoboreshwa.
“Tulipoanzisha TTSA tuliona pengo kubwa la upatikanaji wa mbegu bora. Leo mahitaji yameongezeka zaidi, lakini uwezo wa kuzalisha suluhisho upo, hasa kupitia taasisi kama TFS,” alisema.
Mazungumzo hayo yameibua tena umuhimu wa kuwekeza kwenye sayansi ya mbegu bora, jambo ambalo linatajwa kuwa uti wa mgongo wa misitu inayohitajika kukabiliana na changamoto za ardhi, viwanda vya mazao ya misitu na mahitaji mapya ya kimataifa.
.jpeg)

No comments:
Post a Comment