Na Khadija Kalili, Kibaha
MEYA wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, amesema kuwa uongozi wake pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha wametenga fedha kiasi cha Mil. 900 na kiasi cha Mil. 400 kwa ajili ya madawati ikiwa ni lengo la kuhakikisha watoto wote waliotimiza umri wa kuanza darasa la kwanza wanaanza masomo ifikapo mwakani.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo kwenye Ukumbi wa Mikutano katika Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas amesisitiza kuwa kiasi cha Mil. 900 ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, huku Mil. 400 kimetengwa kwa ajili ya kutengeneza madawati ya wanafunzi watakaoanza masomo ifikapo mwakani 2026.
“Mil. 400 tayari zimeshatoka na baada ya kukamilika tutawaita mjionee mgawanyo wa shule.
“Tutasimamia katika kuhakikisha aliyechukua tenda ya kutengeneza madawati hayo anatengeneza kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha aliyolipwa,” amesema Meya Dkt. Nicas. “Tutasimamia wenyewe na mimi nikiwa kiongozi naahidi kuwa sitatoa wala kupokea rushwa. Na Mhe. Rais anasisitiza hili jambo litekelezwe kwa vitendo, hivyo basi natoa angalizo endapo watatengeneza madawati hayo chini ya kiwango watachukuliwa hatua kali,” amesema Meya wa Kibaha, Dkt. Nicas.
Aidha, Meya wa Kibaha, Dkt. Nicas, amesema kuwa kila kata imepewa kiasi cha Mil. 30 kwa ajili ya kuchonga barabara za mitaani, huku akiwatoa hofu wananchi ambao bado hawajaona maendeleo katika mitaa yao kwamba wasiwe na wasiwasi kwani fedha bado zipo na wanaangalia namna ya kuratibu matumizi yake ili wananchi waweze kupata huduma ya kuchongewa barabara katika mitaa yao ziweze kupitika katika kipindi cha mwaka mzima.
Wakati huohuo, Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas, amewapongeza wananchi wa Kibaha kwa namna walivyoonesha utulivu katika kusherehekea kumbukumbu ya miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania.
“Kwa sasa tunakwenda na slogan ya siku 100 za Mhe. Rais Dkt. Samia ambapo tumeelekezwa watoto waliofikia umri wa kwenda shule waende. Hivyo tumejipanga vizuri, wote waliofaulu darasa la saba hasa Manispaa ya Kibaha wamefaulu kwa kiwango cha asilimia 100; wote watakwenda shule za sekondari, hakuna atakayeachwa.
“Katika Manispaa ya Kibaha awali waliofaulu walikuwa wanafunzi 3,000; sasa idadi imeongezeka na kuwa 6,000. Ndiyo sababu tumelazimika kuongeza madarasa na madawati. Fedha ipo ya kutosha, tunaishukuru serikali yetu kuwa hakuna mtoto atakayekosa nafasi wala kuachwa,” amesema Meya Dkt. Nicas.
“Tunatarajia ndani ya siku 60 ujenzi wa madarasa utakamilika, na ninasisitiza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia anastahili pongezi nyingi kutokana na kufanya maajabu katika kipindi cha uongozi wake kwa kuleta maendeleo mengi na yanayoonekana nchini.”


No comments:
Post a Comment