Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameitaka menejimenti ya Shirika la Posta Tanzania kuongeza ubunifu na kuendelea kujiimarisha kimkakati kwenye mifumo ya kifedha ili kuleta ushindani katika utoaji wa huduma ndani ya nchi na kimataifa.
Waziri Kairuki aliyasema hayo tarehe 27 Novemba, 2025 wakati akizungumza na menejimenti ya Shirika hilo na kusisitiza kuwa posta ya sasa ni “posta mpya” inayopaswa kujikita katika ubunifu na kuendana na mabadiliko ya kasi ya teknolojia. Alitoa wito kwa TPC kujifunza kutoka nchi mbalimbali, kutambua mahitaji ya jamii, kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine, na kuharakisha maboresho ya teknolojia. Aidha, alihimiza kuimarisha ushirikiano na UPU na kuhakikisha utekelezaji wa Data Protection Policy ili kulinda taarifa za wananchi na watumiaji wa huduma.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Shirika, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo, alimweleza Waziri Kairuki historia fupi ya shirika, hali ilivyo sasa, mafanikio yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na huduma zinazotolewa kwa sasa, ikiwemo Swift Pack, Kipepeo (Duka la Mtandao), Posta Kiganjani, huduma za kifedha na za mitandao, sambamba na mwelekeo wa shirika katika miaka mitano ijayo.
Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb) walitembelea maeneo muhimu ya kiutendaji ya shirika na kuijonea mitambo ya ukaguzi wa mizigo, control room, mashine ya HazMat ID — inayotumika kubaini aina ya kemikali kwenye bidhaa ili kujionea kwa vitendo huduma na matumizi ya teknolojia katika kazi za kila siku za shirika.
Postamasta Mkuu pamoja na menejimenti ya shirika walimshukuru Waziri kwa kutenga muda kufanya ziara hiyo, na wakaahidi kuongeza juhudi ili kufikia malengo ya miaka mitano ya shirika, ikiwemo kuwa miongoni mwa kampuni 10 bora nchini katika utoaji wa huduma bora zinazomfikia kila Mtanzania.







.jpeg)


.jpeg)
No comments:
Post a Comment