HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 25, 2025

Viongozi Wapya Maliasili Wataka Utu Katika Uhifadhi, Utalii






Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu wake Mhe. Hamad Chande, wamewataka maofisa na askari wa uhifadhi nchini kuendeleza utu katika kuwahudumia wananchi, kuendeleza uhifadhi na kuwakinga wananch dhidi ya wanyama wakali na waharibifu na kuwakirimu wageni katika utalii.

“Leo tumefika hapa Tawa (Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania), nawapongeza sana na tumekabidhi magari manne, pikipiki 33, bajaji na vitendea kazi kama ndege nyuki (drones), hii yote ni kuonesha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuendeleza uhifadhi.

“Msisitizo wetu mimi na viongozi wenzangu wa Wizara hii ni kwamba Tawa ni moja ya taasisi inayohudumia watu moja kwa moja kule chini. Nawaagiza katika kazi zenu kuanzia kuendeleza uhifadhi, kuwakinga wananchi dhidi ya wanyama wakali na kupokea watalii muendeleze utu na ukarimu,” alisema Dkt. Ashatu.

Naye Naibu Waziri Chande aliwapongeza wahifadhi hao kwa kazi nzuri nchi nzima na kusema viongozi hao wapya wako tayari kushirikiana nao kutatua changamoto mbalimbali.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, aliyewaongoza watumishi wengine kuwapokea viongozi katika ziara yao ya kwanza kwenye taasisi za uhifadhi tangu walipoteuliwa na kuapishwa, amesema pamoja na kuajiriwa wafanyakazi wengi katika miaka hii minne hii kuliko wakati wowote katika sekta hizo, kazi kubwa pia ya wizara hiyo ni kuendeleza ulinzi wa raslimali wanyama:

“Mhe. Waziri pamoja na raslimali watu iliyoongezeka sana katika sekta hii, nataka nikujulishe tu utasimamia pia uhifadhi wa raslimali wanyama wakiwemo simba 17,000; nyati 225,000; tembo 60,000 na chui 24,000 walioko nchi nzima kutaja kwa uchache.”

Viongozi hao wanaendelea na ziara za kujitambulisha katika taasisi mbalimbali za sekta hiyo na kukagua miradi ya utalii inayoendelea kutekelezwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad