Na Janeth Raphael MichuziTv -- Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumanne Novemba 18, 2025 amewaapisha Mawaziri na Manaibu Waziri katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, huku akiwataka viongozi hao kutanguliza uwajibikaji, utu na matokeo chanya katika utekelezaji wa majukumu yao.
Katika hotuba yake, Rais Samia amewakumbusha viongozi hao kuwa dhamana walizokabidhiwa ni jukumu la kufanya kazi kwa niaba ya wananchi, akisisitiza kuwa uongozi si fahari bali wajibu.
“Imani yangu ni kwamba baada ya kuapa mmekubali kuyabeba majukumu yenu kwa moyo mkubwa na kwenda kuwatumikia watu; dhamana mlizopewa ni za kazi na si fahari,” alisema Rais Samia.
Aidha, amewataka Mawaziri na Manaibu Waziri kuonesha mfano wa utu na matumizi sahihi ya mamlaka, akibainisha kuwa kauli mbiu ya serikali ya “Kazi na Utu Tunasonga Mbele” inapaswa kuanzia kwao kabla ya kutekelezwa kwa wananchi.
“Utu uanze na sisi viongozi… tuoneshe utu kwa watu wetu, kujenga utu wao na kuuheshimu utu wa Mtanzania. Hiyo ndiyo kazi yetu,” alisema.
Akiweka msisitizo kwenye uwajibikaji wa haraka, Rais Samia amesema serikali ina ahadi nyingi kwa wananchi huku muda wa utekelezaji ukiwa mfupi, hivyo viongozi wanapaswa kuongeza kasi katika maeneo yao.
“Mambo ambayo tumeahidi kwa wananchi ni mengi mno lakini muda wa kuyatekeleza ni mchache. Kwa hiyo wale mlioapa leo mjue tuna kazi ya kwenda mbio, tena mbio haswa,” aliendelea.
Akizungumzia mwelekeo wa maendeleo katika muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Sita, Rais Samia amesema miradi mingi itaanza kutekelezwa kwa fedha za ndani kabla ya kushirikisha washirika au taasisi nyingine.
“Tutaanza kufanya miradi wenyewe… tutaanza kwa fedha za ndani, kisha wakimaliza taratibu zao watatukuta tukiendelea,” alisema.
Rais Samia amekemea tabia ya kutolea taarifa zisizoonyesha matokeo halisi kwa wananchi, akiwataka viongozi kuhakikisha miradi na kazi zao zinaonekana na kuleta athari chanya katika maisha ya watu.
“Sitaki zile za ‘tunaendelea’ au ‘mchakato uko mbioni’, nataka matokeo — na matokeo hayo yawe kwa wananchi, si ofisini kwako,” alihitimisha.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, watendaji na ndugu wa viongozi walioapishwa.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment