Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 27, 2025. Na kusisitiza kuwa mabadiliko ya taarifa ni sehemu ya huduma za msingi zinazotolewa na NIDA kwa watu waliopo kwenye mfumo wake, lakini kwa muda mrefu baadhi ya maombi yalishindwa kufanyiwa kazi kutokana na matumizi ya nyaraka za kughushi, taarifa za uongo au usajili usiofuata utaratibu.
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, ametoa wito kwa wananchi wenye changamoto za taarifa zao za usajili wa NIDA kujitokeza katika ofisi za wilaya za mamlaka hiyo ili kufanyiwa marekebisho kupitia kibali maalum kilichotolewa na Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Oktoba 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 27, 2025 amesema mabadiliko ya taarifa ni sehemu ya huduma za msingi zinazotolewa na NIDA kwa watu waliopo kwenye mfumo wake, lakini kwa muda mrefu baadhi ya maombi yalishindwa kufanyiwa kazi kutokana na matumizi ya nyaraka za kughushi, taarifa za uongo au usajili usiofuata utaratibu.
“Serikali imetoa kibali maalum cha mwaka mmoja kushughulikia maombi yaliyokwama kwa muda mrefu. Kibali hiki kinahusu makundi maalum ya wananchi ambao awali taarifa zao zilishindwa kusahihishwa kutokana na changamoto mbalimbali,” amesema Kaji.
Ameeleza kuwa, makundi yanayohusika ni pamoja na Waathirika wa vyeti vya kughushi, wakiwemo waliowahi kufukuzwa kwenye ajira za Serikali kutokana na kutumia vyeti vya shule bandia walivyojitambulisha navyo pia kwa NIDA, Watu waliotumia majina ya wengine kupata vyeti vya elimu, Wale waliotoa taarifa za uongo au udanganyifu wakati wa usajili wa NIDA na Raia wa Tanzania waliojisajili kama wakimbizi.
Kaji amesisitiza kuwa waombaji kutoka makundi hayo wanapaswa kufika ofisi za NIDA za wilaya wakiwa na nyaraka muhimu kulingana na aina ya changamoto wanayokabiliana nayo.
Miongoni mwa nyaraka hizo ni pamoja na nakala halisi za vyeti vya elimu, cheti cha kuzaliwa kilichohakikiwa na RITA, deed poll iliyosajiliwa kwenye gazeti la Serikali pamoja na nyaraka nyingine zinazoweza kuhitajika kwa uthibitisho wa taarifa.
“Maombi yatakayofanyiwa kazi ni yale tu yatakayokidhi masharti na vigezo vilivyowekwa. Tunawaomba wananchi kuhakikisha wanakuja na nyaraka sahihi ili kufanikisha marekebisho,” ameeleza.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa muda wa kibali hicho ni maalum na hautaongezwa, hivyo ni muhimu kwa wananchi wenye changamoto za taarifa kujitokeza mapema kabla ya kipindi cha mwaka mmoja kuisha.
Aidha, amewakumbusha wananchi umuhimu wa kutoa taarifa sahihi na za kweli wakati wa usajili wa NIDA, akibainisha kuwa udanganyifu wa taarifa ni kosa kisheria chini ya Sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu.
Kaji amesema kuwa NIDA inatarajia wananchi kutumia fursa hiyo kufanya marekebisho kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, ili kuboresha taarifa zao kwenye Mfumo wa Taifa wa Utambuzi.
Pia ameishukuru Serikali kwa kutoa kibali hicho ambacho kinalenga kushughulikia maombi ya muda mrefu ya mabadiliko ya taarifa yaliyokwama kutokana na kukosa vigezo au kukinzana na miongozo iliyokuwepo awali.



No comments:
Post a Comment