Katika majadiliano hayo, Meneja Wa TRA Dodoma Bw. Pendolake Elinisafi aliwasilisha mikakati yake ya kuimarisha njia rafiki za ukusanyaji wa kodi, ikiwemo kuboresha utoaji wa huduma, kuimarisha mifumo ya TEHAMA kama EFD, kutoa elimu endelevu ya kodi na kushughulikia changamoto kwa misingi ya mazungumzo na ushirikiano. Wadau walipongeza jitihada hizo na kuonyesha matumaini makubwa kwamba maboresho yanayoendelea yataongeza utii wa hiari na kuimarisha mazingira ya biashara mkoani humo.
Wakichangia hoja mbalimbali wadau wa kodi walisisitiza umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya mara kwa mara kati ya TRA na wafanyabiashara. Bwana Gabriel Mauna, mmiliki wa hoteli, alihimiza utoaji wa taarifa sahihi na za kutosha na Elimu ya kodi kwa wafanyabiashara ili kuwawezesha kufuata taratibu za kodi bila usumbufu. Pia alipongeza kwa Maendeleo ya mifumo mbali mbali ya kidigitali na kutoa wito kutoa Elimu zaidi ya mifumo ya ukusanyaji ili kuongeza kasi na ufanisi. Alipongeza hatua ya TRA Dodoma kufungua ofisi katika wilaya mbalimbali, hatua iliyopunguza umbali na gharama kwa walipakodi waliokuwa wakifuata huduma mjini.
Aidha, Bi Grace kutoka TWCC (Tanzania Women Chamber of Commerce) aliunga mkono umuhimu wa ushirikiano endelevu kwa kuomba kikao cha wadau wa kodi kiwe kinaitishwa mara kwa mara ili kujadiliana, kujenga uelewa wa pamoja na kuhakikisha changamoto za kikodi zinapatiwa majawabu ya kudumu. Alisema kufanya hivyo kutachochea ukuaji wa biashara, kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo ya Mkoa wa Dodoma.
Kikao hiki kilipokea maoni na mapendekezo mengi ya kujenga kutoka kwa wadau mbalimbali, yote yakilenga kuimarisha uhusiano kati ya TRA na wafanyabiashara pamoja na kuongeza tija katika ukusanyaji wa kodi. Wadau walionyesha utayari na dhamira ya kuendelea kushirikiana na TRA, wakiahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha Mkoa wa Dodoma unavuka malengo yake ya makusanyo na kuimarisha uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.










No comments:
Post a Comment