KAMPUNI ya bia Tanzania Breweries Plc (TBL), ambayo ni kuwa sehemu ya familia ya AB InBev, leo imefanya maadhimisho ya Global Responsible Beer Day katika mikoa minne: Mwanza, Mbeya, Arusha na Dar es salaam. Siku hii maalum inaadhimishwa kila mwaka duniani kote kwa lengo la kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa unywaji wa pombe kwa uwajibikaji.
Maadhimisho haya ni sehemu ya juhudi endelevu za AB InBev na TBL katika kuimarisha utamaduni wa unywaji kwa kuwajibika, kuelimisha jamii kuhusu madhara ya unywaji kupita kiasi, na kuchochea mabadiliko chanya ya kitabia kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Neema Temba, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na Mahusiano wa TBL, amesema: “Sisi kama wazalishaji wa bia hapa nchini tuna wajibu wa kuikumbusha jamii yetu, hasa wateja wetu wanaofurahia bidhaa zetu, kuhakikisha wanakunywa kistaarabu na kwa kuwajibika. Tunataka kuona jamii inayofurahia bia zetu kwa usalama, bila madhara kwao au wengine.”
Ameongeza kuwa kupitia kampeni ya “Kunywa Mdogo Mdogo”, TBL inahamasisha watumiaji wa vinywaji vyao kufuata vidokezo vifuatavyo:
● Kunywa maji ya kutosha wakati wa kufurahia bia;
● Kula chakula kabla na baada ya unywaji wa pombe;
● Kuepuka kuendesha gari endapo umelewa.
Kwa mujibu wa TBL, ujumbe huu ni sehemu ya dhamira pana ya kampuni hiyo kuhakikisha wateja wake wanafanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya pombe, huku ikiunga mkono jitihada za serikali na wadau wengine katika kupambana na unywaji kupita kiasi.
No comments:
Post a Comment