Serikali imeipongeza Shule ya Sekondari East Coast kwa kuanzisha masomo ya amali, hatua inayokwenda sambamba na maelekezo ya Waziri Mkuu kuhusu kuimarisha elimu ya ufundi na ujuzi mashuleni.
Akizungumza katika mahafali ya shule hiyo, Afisa Elimu wa Sekondari Manispaa ya Kibaha, Isihaka Rashid, alisema uamuzi huo ni mchango mkubwa katika kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa fani mbalimbali zitakazowasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Katika mahafali hayo, wanafunzi walionesha umahiri wao katika fani za mapishi, kilimo, ufundi wa umeme na kuchomelea vyuma, wakithibitisha mafanikio ya programu hiyo ya masomo ya amali.
Mkuu wa Shule hiyo, Paulina Malewo, alisema sambamba na kuimarisha elimu ya amali, wamejipanga kuhakikisha wanaondoa kabisa ufaulu wa daraja la nne katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.
Kwa upande wake, mgeni rasmi wa hafla hiyo, Dkt. Duncan Mwakipesile, ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Ubunifu kutoka Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania, aliahidi kushirikiana na shule hiyo katika kuendeleza elimu ya ujuzi.
“Mashirikiano haya yatasaidia kuhakikisha wanafunzi wanapata stadi zitakazowapa fursa ya kuweza kujiajiri mara baada ya kuhitimu,” alisema Dkt. Mwakipesile.
No comments:
Post a Comment