HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 23, 2025

REA YAHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA TANDAHIMBA

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetoa wito kwa wananchi kutumia Nishati Safi ya Kupikia ili kulinda afya na kuokoa mazingira.

Wito huo umetolewa Oktoba 22, 2025 katika Kijiji cha Chikongola Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara na Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka REA, Jaina Msuya wakati wa kampeni ya kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034.

“Tunawasihi na kuwahamasisha watanzania kutumia nishati safi ya kupikia kwani faida zake ni nyingi zikiwemo kulinda afya na mazingira, kupunguza gharama za maisha na kupata muda wa kufanya shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii kwani nishati safi ya kupikia hutumia muda mfupi kuivisha chakula,” alisisitiza Msuya.

Alisema katika kutekeleza Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, REA inatumia njia mbalimbali katika kuelimisha, kuwezesha na kuhamasisha wananchi ili kufikia lengo la 80% ya wananchi kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo Mwaka 2034.

“Leo hii tumetembelea wajasiriamali wa chakula maarufu kama Mamalishe hapa katika Kijiji cha Chikongola wilaya ya Tandahimba na tumetoa zawadi ya jiko banifu kwa Amina Abdallah ambaye anajishughulisha na biashara ya Mama Lishe na tumehakikisha jiko hilo linaanza kutumika leo ili na wengine waweze kushuhudia ufanisi wake tukiwa hapa,” alisema Msuya.

Kwa upande wake Amina Abdallah, aliipongeza REA kwa uhamasishaji na elimu ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia aliyoipata lakini pia alishukuru kwa zawadi ya jiko banifu aliyopatiwa wakati wa kampeni hiyo.

“Jiko hili nimelipenda kwani nimetumia muda mfupi kuandaa chakula, jiko ni zuri halina athari ya cheche inayoweza kuleta madhara na pia halina moshi hivyo linapunguza athari za maradhi yanayotokana na uvutaji wa hewa chafu,” alifafanua Amina.

Alisema jiko banifu hilo litamsaidia kupunguza gharama ambazo alikuwa akitumia kununua mkaa kwani linatumia mkaa kidogo ikilinganishwa na majiko mengine na kwamba linao uwezo mkubwa wa kutunza joto na hivyo litamwezesha kupika mapishi mbalimbali kwa mkaa kidogo.

Akizungumza wakati wa kampeni hiyo, Musa Mkula Mkazi wa Mahuta, Tandahimba aliipongeza REA kwa jitihada zake za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

“Nimefuatilia wakati hili jiko likiwashwa hadi hatua ya mwisho ya kupakua chakula, nimeshuhudia linafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, tunaomba Serikali itoe majiko haya kwa wingi ili kusaidia kupunguza uharibifu wa mazingira, nimeona limetumia mkaa kidogo ikilinganishwa na majiko mengine,” alifafanua Mkula



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad