HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 23, 2025

Airtel Africa Yasema Ushirikiano ni Nguzo Muhimu katika Kujenga Mustakabali wa Kidijitali wa Afrika

 



Kigali, Oktoba 21, 2025 – Airtel Africa,
KAMPUNI inayoongoza katika huduma za mawasiliano na fedha kwa njia ya simu katika nchi 14 barani Afrika, imesisitiza kuwa ushirikiano wa sekta mbalimbali, matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI), na uendelezaji wa vituo vya kuhifadhia data ni nguzo muhimu katika kujenga mustakabali wa kidijitali wa Afrika.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Bw. Sunil Taldar, maendeleo haya yatachochea mapinduzi ya mawasiliano barani Afrika kwa kubadilisha mtazamo wa teknolojia kutoka kuwa chombo cha kuunganisha watu pekee hadi kuwa nyenzo ya kuongeza thamani na kuibua fursa mpya.

Akizungumza katika Kongamano la MWC25 Kigali, Bw. Taldar alisema“Muongo wa kidijitali wa Afrika umeanza. Bara ambalo limefanikiwa kupiga hatua kubwa katika matumizi ya simu za mkononi sasa liko tayari tena kwa hatua nyingine – kuelekea zama ambapo kila matumizi ya intaneti yanapaswa kuleta tija, na kila jamii iliyounganishwa iweze kujijengea ustawi.”

Aliongeza kuwa“Afrika iko tayari kwa hatua inayofuata – kutoka kwenye upatikanaji wa huduma hadi kwenye ufanisi na ubunifu. Hii inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya watoa huduma wanaojenga miundombinu, watengenezaji wa teknolojia, wasimamizi wa sera, wawekezaji, mifumo ya kodi rafiki, na vijana wabunifu wa Kiafrika. Kwa pamoja, tunaweza kujenga bara ambalo huduma za intaneti zinachakatwa ndani ya bara, vipaji vinakuzwa kitaifa, na ubunifu unasambazwa duniani kote.”

Bw. Taldar pia alisisitiza kuwa mustakabali wa kidijitali wa Afrika unahitaji matumizi ya AI ili kuboresha mitandao, kuongeza ufanisi wa huduma, kuboresha uzoefu wa wateja, na kuimarisha usalama wa huduma za fedha kwa njia ya simu. Ili kufanikisha haya, bara linahitaji mtandao wa vituo vya data vilivyounganishwa kwa nyaya za kasi ya juu, ambavyo vitawezesha upatikanaji wa huduma hata katika maeneo ya pembezoni.

Akitolea mfano, alisema Airtel Africa inawekeza katika vituo vikuu vya data nchini Nigeria na Kenya ili kusaidia mustakabali wa kidijitali wa Afrika. Kampuni pia inatumia AI kubaini ujumbe wa ulaghai (spam), kusajili wateja, na kuboresha matumizi ya nishati safi kwenye minara ya mawasiliano.

Kongamano la mwaka huu la MWC25 Kigali limewakutanisha viongozi wa sekta, wabunifu, na watunga sera, likiwa na lengo la kuangazia namna teknolojia ya mawasiliano ya kidijitali inavyoweza kuharakisha mabadiliko ya bara la Afrika.

Mheshimiwa Rais wa Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame, alipolizindua rasmi kongamano hilo, alisema:“Afrika imepiga hatua kubwa kutoka kuwa na miundombinu michache ya mawasiliano hadi kuwa na uchumi unaoendeshwa na teknolojia ya simu za mkononi. Ingawa changamoto bado ni nyingi, pia kuna fursa kubwa za ukuaji endapo tutashirikiana.”

Aliongeza kuwa:“Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wanapaswa kuoanisha sera na kuunda mazingira rafiki kwa ubunifu. Hii itarahisisha mifumo yetu ya data na malipo kuvuka mipaka kwa usalama na kuunganisha uchumi wetu. Mustakabali tunaopaswa kuujenga ni wa Afrika yenye ujasiri, iliyounganishwa na yenye ushindani.”

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad