Na Emmanuel Massaka Pemba
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Mtambile, Mkoa wa Kusini Pemba, Mheshimiwa Mohamed Abdallah Kassim, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema kuwa hali ya kisiasa katika jimbo hilo ni ya amani na furaha, kwani ni sherehe za ushindi ndizo zinaendelea, siyo maandamano.
Akizungumza katika mwendelezo wa kampeni za CCM zinazoendelea jimboni humo, Mheshimiwa Mohamed alisema wananchi wa Mtambile wameonyesha imani kubwa kwa chama hicho na wako tayari kuipa ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao.
“Wananchi wa Mtambile wanajua mazuri yaliyofanywa na serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hivyo, ni furaha na shangwe za ushindi zinazotawala, hakuna dalili yoyote ya maandamano,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi waendelee kuiamini CCM kwa kuwa ni chama pekee kilichoonyesha uthabiti katika kuwaletea maendeleo Watanzania wote bila ubaguzi.
“Naomba tuendelee kushikamana, tuiunge mkono CCM kupitia kura zetu, kwani kwa pamoja tutaendelea kusonga mbele katika maendeleo,” alisisitiza.
Mheshimiwa Mohamed aliongeza kuwa wananchi wa Mtambile wako tayari kumpa kura Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ili waendelee kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
No comments:
Post a Comment