Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuendeleza elimu ya juu yenye matokeo chanya katika uchumi wa Taifa, kupitia utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaofadhiliwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia.
Akizungumza Oktoba 22,2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, ameipongeza Serikali kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 18 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo muhimu unaolenga kuifanya elimu ya juu kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Mradi wa HEET unaleta mageuzi makubwa katika namna tunavyoiendesha elimu ya juu nchini. Elimu haitabaki vitabuni, bali itakuwa chombo cha kuzalisha ubunifu na suluhisho kwa changamoto za wananchi,”amesema Dkt. Nungu.
Kupitia mradi wa HEET, COSTECH imefanikiwa kukarabati jengo lake la makao makuu jijini Dar es Salaam, pamoja na ujenzi wa Jengo la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STI Complex) jijini Dodoma, ambalo linatarajiwa kuwa kitovu cha ubunifu, tafiti na maendeleo ya teknolojia nchini.
Dkt. Nungu alibainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi wanaoshiriki katika miradi hii ni Watanzania, hatua inayochochea ajira na kukuza uchumi wa ndani.
Katika hatua nyingine, COSTECH inaendelea kutengeneza Mfumo wa Kitaifa wa Uratibu wa Taarifa za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (NISSTI), unaolenga kukusanya, kuchakata na kusambaza takwimu za sekta ya utafiti na ubunifu nchini.
Utekelezaji wa mfumo huu umefikia asilimia 40, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba 2025. Mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa takwimu muhimu kwa watunga sera, watafiti na wawekezaji.
Kupitia HEET, COSTECH imetoa mafunzo kwa taasisi 10 za elimu ya juu kuhusu kuanzisha na kuimarisha Ofisi za Uhawilishaji wa Teknolojia (TTOs) ambazo zinasaidia kuziba pengo kati ya utafiti na biashara.
Matokeo yake, maombi 10 ya hati miliki (patents) yamepitishwa na BRELA, huku maombi mengine 29 yakiwasilishwa. Pia, bunifu 12 kutoka vyuo vya MUHAS, UDOM, NM-AIST, MU na UDSM zimewezeshwa kifedha, na tayari bidhaa 4 za mfano (MVPs) zimezalishwa, moja ikiwa imepata ufadhili wa CRDB Foundation kwa maendeleo zaidi.
Mradi wa HEET pia umeboresha Mtandao wa Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti (HERIN), unaotoa huduma ya intaneti yenye ubora wa hali ya juu kwa taasisi 14 za elimu ya juu na vyuo 15 vya ualimu wa ufundi.
Kwa sasa, HERIN imeongezewa huduma ya bure ya mikutano kwa njia ya video, jambo lililoongeza ufanisi katika ufundishaji, utafiti, na ushirikiano wa kitaaluma.
Dkt. Nungu alisisitiza kuwa juhudi hizi hazitaishia kwenye mradi wa HEET pekee, bali zitakuwa endelevu ili kuhakikisha ubunifu, utafiti na teknolojia vinakuwa uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.
“Chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, serikali imeweka msingi imara wa mageuzi ya elimu ya juu. Tunachokifanya leo ni kuandaa vizazi vya wabunifu, wanasayansi na wataalamu watakaolijenga taifa letu kiuchumi,”alisema.
Wednesday, October 22, 2025

Home
Unlabelled
HEET Yaibua Mageuzi Makubwa Katika Sekta ya Elimu ya Juu Tanzania
HEET Yaibua Mageuzi Makubwa Katika Sekta ya Elimu ya Juu Tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment