MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amewataka Watanzania kujivunia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, akisema ameleta mageuzi makubwa katika sekta ya utalii na kuifanya Tanzania kuwa moja ya vivutio vinavyoongoza Afrika.
Akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika Mkuranga mkoani Pwani, juzi jioni, Dk Nchimbi alisema katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Rais Samia, idadi ya watalii imeongezeka kwa kiwango kisicho na mfano kutoka watalii 620,000 hadi kufikia milioni 5.3.
“Ni jambo la kujivunia kuona namna Rais Samia alivyoibadilisha sekta ya utalii. Kutoka watalii 620,000 hadi milioni 5.3 si jambo dogo. Hii ni kazi kubwa iliyofanywa kwa weledi, juhudi na kuipa sekta hii msukumo mpya. Kama hili lingekuwa jaribio, basi mama yetu angepata alama 100 kwa 100,” alisema.
Alisema mafanikio hayo ni ushahidi wa uongozi madhubuti na dira sahihi ya Rais Samia katika kuleta maendeleo ya kweli kwa taifa.
Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, matokeo hayo pia ni kielelezo cha utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025, ambayo imeleta mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
“Miaka mitano imetimia tangu uchaguzi wa 2020. Sasa tunaomba idhini kwa wananchi watuchague tena. Tuna ujasiri kusimama mbele yenu leo kwa sababu tuna rekodi ya utekelezaji mzuri wa Ilani yetu chini ya Rais Samia,” alisema.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo yameenda sambamba na kuimarika kwa amani, utulivu na mshikamano wa taifa, huku serikali ikiendelea kuwekeza kwenye majeshi kwa mafunzo na vifaa vya kisasa.
“Kwa Watanzania, jambo muhimu ni amani na mshikamano. Leo hii nchi yetu iko imara na salama. Rais Samia amefanikisha hilo kwa asilimia 100,” alisema.
Akizungumzia maendeleo ya Wilaya ya Mkuranga, Dk Nchimbi alisema Serikali ya CCM imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za afya, elimu, kilimo, nishati, maji na miundombinu.
Alisema katika miaka mitano ijayo chama hicho kimekusudia kuiboresha zaidi Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kwa kuongeza wataalamu na vifaa tiba, na ujenzi wa zahanati tisa, vituo vya afya vitano na nyumba sita za watumishi wa afya.
Kwa upande wa elimu, alisema shule mpya tatu za msingi zitajengwa, shule nne za sekondari za zamani zitaboreshwa, madarasa 135 ya shule za msingi na madarasa 52 ya sekondari yataongezwa, huku mabweni mapya 45 yakijengwa ili kuboresha mazingira ya wanafunzi.
Kwenye kilimo, Serikali itaimarisha skimu za umwagiliaji, kujenga ghala kubwa la kuhifadhi chakula, kuanzisha minada mitatu, kuongeza maofisa ugani na kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za ruzuku pamoja na dawa za kilimo.
Aidha, alisema serikali imepanga kuhakikisha vitongoji 89 vilivyobaki katika Wilaya ya Mkuranga vinapata umeme ndani ya miaka mitano ijayo, na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo yote.
“Nawapongeza wananchi wa Mkuranga kwa kulifanya eneo hili kuwa kitovu cha viwanda nchini. Hii ni dalili tosha kuwa mko tayari kupokea fursa zaidi za maendeleo,” alisema.
Alisema Wilaya ya Mkuranga imepata mafanikio makubwa ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya, umeme katika vijiji vyote, ujenzi wa viwanda, miradi ya maji, mikopo kwa akinamama na vijana, na kupungua kwa bei ya salfa kutoka Sh. 20,000 hadi Sh. 15,000.
“Mkuranga imepata VETA, miradi ya barabara na viwanda vingi. Pwani inaongoza kwa viwanda, lakini Mkuranga ndio nyumbani kwa viwanda,” alisisitiza.
Aidha, alisema bado kuna mambo kadhaa yanayohitaji msukumo zaidi ikiwemo upanuzi wa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Mkuranga kuwa njia nne, ujenzi wa kituo kikubwa cha mabasi yaendayo kusini na kuendelezwa kwa Bandari ya Kisiju ili kuchochea uchumi.
No comments:
Post a Comment