HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 6, 2025

I&M BANK TANZANIA YAZINDUA KADI YA KWANZA YA WORLD ELITE DEBIT MASTERCARD NCHINI


Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam, Oktoba 1, 2025
KATIKA kuadhimisha miaka 15 ya uwepo wake nchini Tanzania, I&M Bank Tanzania kwa ushirikiano na Mastercard imezindua rasmi bidhaa mpya tatu za kadi za kibenki, ikiwemo World Elite Debit Mastercard, kadi ya kwanza aina yake nchini Tanzania.

Uzinduzi huo wa kihistoria ulifanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi wa sekta ya fedha na wageni mashuhuri akiwemo Bw. Thomas Mwongela, Meneja wa Usimamizi na Sera wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na Bw. Shehryar Ali, Makamu wa Rais Mwandamizi na Meneja wa Nchi wa Mastercard kwa Afrika Mashariki na Visiwa vya Bahari ya Hindi.

Ushirikiano huu wa kimkakati unaashiria hatua kubwa katika kuendeleza huduma za kifedha zenye usalama, urahisi na ubunifu, sambamba na mwelekeo wa Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.

World Elite Debit Mastercard ni kadi ya malipo ya hadhi ya juu (premium debit card) inayolenga wateja wanaotaka huduma za kifahari, za kimataifa na zenye thamani halisi. Kadi hii inatoa manufaa ya kipekee yanayojumuisha:

Ufikiaji usio na kikomo katika zaidi ya 1,700 maeneo ya mapumziko ya viwanja vya ndege (airport lounges) katika zaidi ya nchi 70 duniani kote;

Bima kamili ya safari, ikiwemo ucheleweshaji wa safari, kupotea kwa mizigo au usumbufu wa usafiri;


Punguzo maalum katika zaidi ya viwanja 100 vya gofu duniani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Zahid Mustafa, Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank Tanzania alisema:

“Wateja wa leo wanahitaji zaidi ya kadi tu wanataka thamani, uaminifu na huduma zinazokubalika kimataifa. Kupitia uzinduzi wa kadi hizi tatu, World Elite Debit, Gold Debit, na Multi-Currency Platinum Prepaid, tunawapa wateja wetu uzoefu wa kidijitali ulio rahisi, manufaa ya kipekee na amani ya akili.”

Mbali na World Elite Debit Mastercard, I&M Bank imezindua pia bidhaa mbili mpya za kadi ambazo ni I&M Mastercard Multicurrency Prepaid Card, Kadi ya kwanza nchini Tanzania yenye uwezo wa kutumia sarafu 8 tofauti katika kadi moja. Ambayo inawawezesha wateja kusafiri, kununua na kufanya miamala kimataifa kwa urahisi bila kubadilisha sarafu mara kwa mara,

I&M Mastercard Gold Debit Card, Kadi salama na rahisi kwa matumizi ya kila siku, ikiruhusu miamala ya ndani na kimataifa moja kwa moja kutoka kwenye akaunti ya mteja.

Kwa mujibu wa Simon Gachahi, Mkuu wa Benki ya Rejareja na Kidijitali wa I&M Bank Tanzania alisema,

 “Bidhaa hizi zimetengenezwa mahsusi kwa wataalamu wanaopokea mishahara, vijana wa kidijitali, wasafiri wa mara kwa mara na watu wenye hadhi ya kifedha ya juu wanaotafuta suluhisho bora, salama na linalokubalika kimataifa.”

Kwa upande wake, Shehryar Ali, Makamu wa Rais Mwandamizi na Meneja wa Nchi wa Mastercard alisema,

“Mastercard inajivunia kushirikiana na I&M Bank kuzindua kadi hizi mpya zenye manufaa ya kipekee kwa wateja. Tunajitolea kuendeleza mfumo wa malipo wa kidijitali nchini Tanzania kupitia ushirikiano wa kimkakati kama huu. Kupitia teknolojia ya Mastercard, wateja wa I&M Bank watanufaika na urahisi, usalama, huduma zinazokubalika duniani kote, pamoja na ofa na zawadi za mara kwa mara.”

Uzinduzi wa kadi hizi ni sehemu ya mkakati mpana wa I&M Bank Tanzania wa kuimarisha huduma za kifedha kupitia teknolojia, kuboresha uzoefu wa wateja na kuongeza usalama katika miamala ya kimtandao.

Kwa kuanzisha World Elite Debit Mastercard, Tanzania sasa inajiunga na mataifa machache barani Afrika yanayotoa huduma za kadi za hadhi ya juu kwa wateja wake, hatua inayodhihirisha ukuaji wa sekta ya kifedha na maendeleo ya ubunifu wa kidijitali nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad