Na Khadija Kalili
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Hassan Serera, amewataka wahitimu wa mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Taasisi za Umma (SLM-PESA) pamoja na vijana kwa ujumla, kuzingatia afya ya akili ya wafanyakazi na wale wanaowaongoza katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza kama mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo hayo ya siku sita, yaliyofanyika kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 4 mwaka huu katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha, mkoani Pwani, Dkt. Serera alisisitiza kuwa viongozi wana jukumu la kutumia hekima na maarifa waliyopata kukabiliana na changamoto ya afya ya akili sehemu za kazi.
“Ukiwa kiongozi mnao wajibu wa kuzingatia elimu mliyopatiwa ili kukabiliana na changamoto hii, ambayo bado haijapewa uzito wa kutosha. Tafuteni njia za hekima kuitatua,” alieleza Dkt. Serera.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yawe chachu ya kugundua na kusaidia wale wenye changamoto za afya ya akili kwa hekima na utu, badala ya kutumia njia kali zisizoleta suluhisho.
“Kuandika barua kali na kutoa maonyo siyo suluhisho sahihi. Lugha za ukali huzidisha tatizo. Tafuteni njia mbadala, zungumzeni nao kwa uelewa,” alisisitiza.
Dkt. Serera aliwahimiza wahitimu kuhakikisha wanaitendea haki elimu waliyoipata kwa kuitekeleza kwa vitendo katika maeneo yao ya kazi.
Kwa upande wake, Veronica Marwa, akizungumza kwa niaba ya wahitimu 29 wa mafunzo hayo, alisema wamepata maarifa mengi yatakayowasaidia kuwa viongozi bora.
“Tulivyoingia ni tofauti na tunavyotoka. Tumejifunza uongozi wa kimkakati, uzalendo, ulinzi wa rasilimali za nchi – ambazo ni chakula cha taifa – pamoja na itifaki na mambo mengine mengi,” alisema Marwa, akiomba mafunzo hayo yawe endelevu.
Naye John Baitani, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Shule hiyo, Prof. Marcellina Mvula Chijoriga, alisema kuwa shule hiyo ilipokea maombi 300 ya kushiriki mafunzo, lakini ni wahitimu 29 pekee walioweza kujigharamia, licha ya wengi kuonesha nia ya dhati.
“Tangu kuanzishwa kwa shule hii, tumeshaendesha zaidi ya mafunzo 60 na kuwahudumia wahitimu takribani 14,000,” alifafanua Baitani.
Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere inamilikiwa na vyama sita rafiki vya Kusini mwa Afrika ambavyo ni: CCM (Tanzania), MPLA (Angola), SWAPO (Namibia), ZANU-PF (Zimbabwe), ANC (Afrika Kusini) na FRELIMO (Msumbiji). Mdhamini mkuu wa shule hiyo ni Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC).
No comments:
Post a Comment