HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 9, 2025

DC WANGING'OMBE AFUNGA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA GHASIA KWA ASKARI WA TAWA

 



📍 Aridhishwa na umahiri wa Askari hao

Na. Beatus Maganja, Njombe.
MKUU wa Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe. Zacharia Mwansasu, Oktoba 8, 2025 amefunga rasmi mafunzo siku 10 ya kukabiliana na ghasia (Anti-Riot) kwa kikosi maalum cha Askari 60 wa mwitikio wa haraka wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA (RRT) katika Kituo cha Mafunzo cha Welela Mkoani Njombe, akisisitiza umuhimu wa nidhamu, weledi na uzingatiaji wa sheria katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mhe. Mwansasu alisema "Serikali inatambua changamoto zinazowakabili Askari wa Uhifadhi, ikiwemo hatari wanazokutana nazo katika kulinda rasilimali za taifa, ambapo baadhi wamejeruhiwa na wengine kupoteza maisha." Na kuongeza kuwa mafunzo hayo yaliyotolewa na TAWA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi yatasaidia kuongeza ufanisi na uwezo wa askari kukabiliana na ghasia kwa kutumia nguvu ya kadiri bila kuathiri haki za binadamu.

Mhe. Mwansasu alieleza kuridhishwa na umahiri uliooneshwa na Askari hao katika mafunzo ya vitendo, yakiwemo matumizi ya mabomu ya machozi, upekuzi, ukamataji watuhumiwa na mazoezi ya ukakamavu. Alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kutoa mafunzo hayo na kuomba kuendeleza ushirikiano huo ili kuboresha utendaji wa Jeshi la Uhifadhi.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alitumia fursa hiyo kulaani vikali vitendo vya baadhi ya wananchi kuvamia na kuwashambulia Askari wa Uhifadhi wakiwa kazini. Aliwataka wananchi kuacha mara moja kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuheshimu sheria za uhifadhi.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Mwansasu aliipongeza Menejimenti ya TAWA kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwataka wahitimu kutumia ujuzi walioupata kuboresha uhifadhi na kuongeza mapato kupitia utalii.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi – Huduma za Shirika, Thabit Maarufu, ambaye alimwakilisha Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha TAWA kifedha na kwa rasilimali watu, jambo linalozidi kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi nchini.

Aidha, Naibu Kamishna Maarufu alitoa shukrani kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, kwa kuruhusu wataalamu wa jeshi hilo kushiriki katika kutoa mafunzo ya kukabiliana na ghasia kwa Askari wa Uhifadhi. Alisema ushirikiano huo ni kielelezo cha mshikamano wa taasisi za ulinzi na usalama katika kulinda rasilimali za taifa.

Akizungumzia mipango ya mbele, alibainisha kuwa TAWA imeandaa mpango maalumu wa kuboresha mfumo wa mafunzo kwa kuongeza kozi mbalimbali ikiwemo mafunzo ya uokoaji majini na kuogelea kwa askari wake, ili kuwaongezea uwezo wa kukabiliana na changamoto katika maeneo mbalimbali ya uhifadhi.

Vilevile, alisema mamlaka imepanga kuongeza vifaa, kuboresha miundombinu ya mafunzo, na kuhakikisha Kituo cha Mafunzo cha Welela kinajengewa uwezo wa kuwa kituo bora na cha mfano nchini katika kutoa mafunzo ya kiusalama na uhifadhi.

Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa TAWA, Abraham Jullu, amelishukuru Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori Duniani (WCS) Kwa mchango wake mkubwa linalotoa Katika shughuli za uhifadhi nchini hususani uwezeshaji wa mafunzo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya RRT yanayolenga kuimarisha uwezo na umahiri wa Askari hao katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi.

Aidha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Asel Mwampamba aliishukuru TAWA kwa kutambua mchango wa Jeshi la Polisi katika kutoa mafunzo hayo, akisisitiza kuwa ushirikiano huo utaendelea kuimarisha nidhamu, ufanisi, na weledi katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi nchini.

Kadhalika, Mratibu wa ulinzi wa program ya Ruaha Katavi WCS Bw. Stanley Mbilinyi alisema Shirika hilo linajivunia kushirikiana kwa ukaribu na TAWA katika kuanzisha na kuunga mkono vikosi vya kwanza vya RRT nchini Tanzania tangu mwaka 2015, pamoja na kushirikiana na taasisi hiyo kuandaa nyaraka muhimu za mipango na kujenga uwezo wa kutekeleza mbinu hii kitaifa.











No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad