HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 8, 2025

WAZALISHAJI NA WASAMBAZAJI WA UNGA WA MAHINDI WAELIMISHWA KUHUSU KANUNI ZA UONGEZAJI VIRUTUBISHO DAR

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa mafunzo kwa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa unga wa mahindi kwa lengo la kuhakikisha bidhaa hiyo inakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, hususani katika uongezaji wa virutubishi.

Mafunzo hayo yameanza kutolewa Septemba 8, 2025 katika vituo vitatu vya jiji la Dar es Salaam (Ubungo, Kinondoni na Temeke) na yataendelea hadi Septemba 16, 2025, ambapo kila kituo kitahusisha mafunzo ya siku mbili.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo leo September 8,2025 jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango wa TBS, Bw. David Ndibalema, alisema dhamira kuu ni kuwapa wadau elimu ya kutosha kuhusu utekelezaji wa kanuni za uongezaji virutubishi kwenye unga wa mahindi unaosindikwa na kuuzwa sokoni.

“Kanuni za uongezaji wa virutubishi kwenye chakula cha aina hii ni za lazima. Zitatumika kwa unga wa ngano, unga wa mahindi, mafuta ya kula yaliyosafishwa pamoja na chumvi.amesema Bw. Ndibalema.
Aidha amesema kuwa, elimu hiyo itawasaidia wazalishaji na wasambazaji kujua wajibu wao na kuchukua hatua sahihi ili kulinda afya za watumiaji na pia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa usajili wa bidhaa.

“Mafunzo haya ni endelevu, TBS itaendelea kutoa mafunzo ya namna hii kwa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wengine wa bidhaa za unga wa mahindi katika mikoa mingine kwa utaratibu huu ambao unafanyika“ amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wasambazaji wa Nafaka Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Emmanuel Benjamin, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yataongeza uelewa wa wadau na kupunguza malalamiko ya wateja.

“Tunapongeza TBS kwa hatua hii. Ni vyema elimu hii pia ikiwafikia na wazalishaji wa bidhaa za nafaka ili wasambazaji tupokee bidhaa bora tayari kwa soko. Hatua hii itasaidia kuimarisha biashara na kuridhisha wateja wetu,” amesema Bw. Benjamin.

Naye, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bw. Tablan Shabani, amesema elimu waliyopata itawasaidia katika kuhakikisha bidhaa wanazozalisha na kusambaza zinakuwa na ubora unaotakiwa.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuimarisha uelewa wa wadau wa nafaka nchini na kuhakikisha unga wa mahindi unaouzwa sokoni unakidhi viwango vinavyotakiwa na kuleta tija kwa wananchi.










No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad