Na Mwandishi Wetu.
Babati, Septemba 2025: Kampuni ya Mati Super Brands Ltd kupitia taasisi yake ya kijamii, Mati Foundation, imezindua rasmi mradi mkubwa wa ugawaji wa pikipiki za magurudumu matatu zinazotumia nishati ya umeme kwa watu wenye ulemavu nchini, ili kuwawezesha kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi zaidi.
Katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika wilayani Babati, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, David Mulokozi, alisema watu wenye mahitaji maalumu wanapaswa kuwekewa mazingira bora ya kujiletea maendeleo ili waweze kuchangia kwa tija kwenye uchumi wa taifa.
“Tumekabidhi pikipiki kwa ajili ya ndugu zetu wenye ulemavu hasa wale wanaojishughulisha, ili ziwasaidie katika shughuli zao na hivyo kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa taifa letu,” alisema Mulokozi.
Wanufaika wa mpango huo, akiwemo Bi Aisha Wenga na Ramadhani Omari wa Babati, waliishukuru Mati Foundation kwa msaada huo, wakieleza kuwa utaleta chachu kubwa ya maendeleo katika maisha yao ya kila siku.
“Nimekuwa nikihangaika kufuatilia madeni ya biashara yangu ya mahindi kwa kutumia usafiri wa kukodi. Sasa kwa pikipiki hii itarahisisha kazi zangu na kupunguza gharama,” alisema Ramadhani kwa furaha.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Mati Foundation, Isack Piganio, alisema taasisi hiyo imekuwa ikitoa sehemu ya faida yake kurudisha kwa jamii kupitia miradi mbalimbali ya kijamii, huku ugawaji wa pikipiki ukiwa ni moja ya hatua za kivitendo za kusaidia makundi maalumu.
No comments:
Post a Comment