Na Mwandishi Wetu, Arusha.
Chama cha Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA Tanzania) kimeitaka Serikali kuharakisha mchakato wa kuandaa sheria mahsusi ya ukaguzi wa ndani ili kuimarisha utendaji kazi wao, kuongeza uwajibikaji na kupunguza mianya ya matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Akizungumza jana jijini Arusha kwenye mkutano wa 12 wa viongozi wa mashirika na taasisi za ukaguzi wa ndani, Rais wa IIA Tanzania, Dkt. Zelia Njeza, alisema changamoto kubwa inayokwamisha maendeleo ya taaluma hiyo ni kutokuwepo kwa mfumo wa kisheria unaotambua na kusimamia kazi za wakaguzi wa ndani.
“Kwa sasa wakaguzi wa ndani wanafanya kazi chini ya mifumo ya taasisi walizoajiriwa bila mwongozo wa kisheria unaowawezesha kufanya kazi kwa uhuru na kulinda maslahi ya umma. Hali hii inafanya mapendekezo yao mara nyingi kubaki bila utekelezaji,” alisema Dkt. Njeza.
Aidha, alisisitiza kuwa sheria hiyo ikipatikana italeta uwiano wa kitaifa katika majukumu ya ukaguzi wa ndani, kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za umma na binafsi, pamoja na kuongeza nidhamu ya matumizi ya fedha.
Vilevile, Njeza aliiomba serikali kuitambua rasmi cheti cha kimataifa cha Ithibati ya Ukaguzi wa Ndani (CIA), ambacho tayari kinatambulika na kuheshimika duniani, ili kuongeza hadhi na weledi wa wakaguzi wa ndani wa Tanzania.
Akifungua mkutano huo ulioshirikisha zaidi ya viongozi na wataalamu 400, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Selemani Mkomi, alisema serikali imesikia changamoto hizo na italifanyia kazi suala hilo.
Hata hivyo, aliwataka wakaguzi wa ndani kuhakikisha wanatanguliza maadili, weledi na nidhamu ya hali ya juu katika majukumu yao, ili kuepuka hati zenye mashaka pindi wakaguzi wa nje wanapokagua taasisi zao.
“Sekta ya ukaguzi wa ndani ni nyeti sana. Serikali inawategemea ninyi kuhakikisha mali na fedha za umma zinasimamiwa vizuri. Fanyeni kazi zenu kwa maadili na uadilifu wa hali ya juu,” alisema Mkomi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mkutano huo, Jonathan Ngoma, alisema lengo la kikao hicho ni kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuimarisha uongozi katika sekta ya ukaguzi wa ndani.
“Tunazungumzia uongozi bora, matumizi sahihi ya rasilimali, uwazi na uwajibikaji. Pia tunawapa viongozi elimu ya namna ya kuwasimamia na kuwaunga mkono wakaguzi wa ndani walioko chini yao ili kuongeza tija kwa taasisi,” alisema Ngoma.
Mkutano huo umehudhuriwa na wakuu wa bodi, wakurugenzi, viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment