Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv – Dodoma
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) limetangaza kuwa Serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imetenga dola za Kimarekani milioni 9.6 (sawa na shilingi bilioni 23.6) katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya huduma za uzazi wa mpango.
Akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uzazi wa Mpango, yaliyoadhimishwa Septemba 26, Mkurugenzi Mkaazi Msaidizi wa UNFPA, Dkt. Majaliwa Marwa, alisema hatua hiyo ni suluhu baada ya kupungua kwa ufadhili, hususan kufuatia kujiondoa kwa USAID.
Alifafanua kuwa fedha hizo zimetolewa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, UNFPA, Gates Foundation, Jamhuri ya Finland, Serikali ya Uingereza (FCDO) na Sweden.
“Uzazi wa mpango siyo dawa pekee, bali ni chaguo. Ni kumpa msichana mdogo nguvu ya kuamua lini aanze familia yake ili ndoto zake zisikatishwe na ujauzito usiopangwa,” alisema Dkt. Marwa.
Katika hotuba yake, alisimulia kisa cha msichana mwenye ndoto ya kuwa mwalimu, ambaye maisha yake yalibadilika kutokana na ujauzito usiopangwa. “Hii si hadithi ya kufikirika,” alisisitiza, “ni uhalisia wa maelfu ya wasichana nchini Tanzania. Kwa huduma bora za uzazi wa mpango, ndoto hizo zinaweza kuokolewa.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Marie Stopes Tanzania (MST), Patrick Kinemo, alisema licha ya changamoto za kifedha, shirika lake liliendelea kutoa huduma katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Mwaka jana tulifanikiwa kuwafikia watu milioni 2.1. Lakini kuanzia mapema mwaka huu, baada ya USAID kujitoa, tumekumbana na changamoto kubwa ya kifedha.
Hata hivyo, tunajaribu kufunika pengo hilo kupitia huduma zetu za kibiashara na bidhaa tunazouza, ili kusaidia wale wasioweza kumudu gharama,” alisema.
Aliongeza kuwa tafiti zinaonyesha kila dola moja inayowekezwa katika uzazi wa mpango inarudisha manufaa ya kiafya na kiuchumi mara 120 zaidi. “Kuwekeza katika uzazi wa mpango ni njia bora ya kupunguza vifo vya akina mama na watoto na kuchochea ukuaji wa uchumi,” alisema Kinemo.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Mama na Uzazi, Dkt. Mzee Nassoro, alisema serikali itaendelea kusimama imara kuhakikisha huduma hizo haziathiriki kutokana na changamoto za ufadhili.
“Takwimu zinaonyesha matumizi ya njia za kisasa yalishuka kutoka asilimia 32 mwaka 2015 hadi asilimia 31 mwaka 2022, jambo hili ni hatari. Tukiongeza kiwango hiki, tungepunguza vifo vya uzazi kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Dkt. Nassoro alibainisha kuwa wizara ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha huduma za uzazi wa mpango zinajumuishwa kwenye bima ya afya kwa wote, hatua itakayosaidia wananchi wengi kupata huduma kwa urahisi.
Aidha, alisema serikali inatumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kufikisha elimu kwa vijana. “Tunawahimiza vijana wasitumie mitandao kwa burudani pekee, bali pia kwa kupata maarifa ya afya na maisha yao,” alisema.
Uzazi wa mpango umetajwa kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa, huku hatua ya serikali na mshikamano wa wadau wa maendeleo ikielezwa kama kinga madhubuti ya kuendeleza huduma hizi.
“Kuwekeza kwa vijana ndiyo uwekezaji bora wa taifa,” alihitimisha.
No comments:
Post a Comment