HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 26, 2025

UDASA Yaandaa Mdahalo wa Vyama vya Siasa Kuhusu Ilani za Uchaguzi Mkuu 2025

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

JUMUIYA ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) imetangaza kuandaa mdahalo wa wazi wa kisiasa utakaohusisha Makatibu Wakuu wa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa lengo la kujadili ilani zao na kutoa fursa kwa wananchi kuzifahamu kwa kina.

Mdahalo huo umepangwa kufanyika Septemba 28, 2025 katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pia utarushwa mubashara kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Akizungumza na vyombo vya habari, Mwenyekiti wa UDASA, Dkt. Elgidius Ichumbaki, amesema lengo la mdahalo huo ni kuwakutanisha wanataaluma, wananchi na viongozi wa vyama ili kusikiliza na kuchambua sera zinazopendekezwa na vyama husika.

“Mdahalo huu utatoa fursa kwa wananchi na wanataaluma kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kutoka kwa viongozi wa vyama kuhusu mipango yao endapo watapata ridhaa ya kuiongoza Tanzania,” amesema Dkt. Ichumbaki.

Vyama 18 vilivyopata vibali kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 vimealikwa kushiriki mdahalo huo, ikiwemo CCM, ACT-Wazalendo, CUF, NCCR-Mageuzi, CHAUMA, ADC, CCK, UDP, TLP, NLD, UMD, DP, SAU, AAFP, MAKINI, ADA-TADEA, NRA na UPDP.

Aidha, wanazuoni mashuhuri watashiriki kama wachambuzi wa mdahalo huo akiwemo Dkt. Victoria Makulilo kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Dkt. Ayub Rioba, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Kwa mujibu wa ratiba, kila Katibu Mkuu wa chama atapewa nafasi ya kueleza malengo makuu ya chama chake, kisha wachambuzi watajadili hoja hizo na kutoa changamoto. Baada ya hapo, maswali kutoka kwa wananchi yatapokelewa kabla ya kufungwa rasmi kwa mdahalo.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad