Dar es Salaam, Septemba 18, 2025
KATIBU Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bw. Patience Ntwina, amesema uchaguzi ni mchakato wa kidemokrasia unaopaswa kuendeshwa kwa misingi ya amani, uhuru na heshima kwa haki za binadamu. Amezitaka taasisi zote kuhakikisha kuwa haki hizo zinalindwa na kutekelezwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora, Bw. Ntwina amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa maafisa kuhusu wajibu wao wa kulinda haki za wananchi na kuwezesha uchaguzi huru na wa haki.
“Mafunzo haya yanalenga kuongeza uelewa wa Maafisa wa Jeshi la Polisi kuhusu nafasi yao katika kulinda haki za wananchi na kuhakikisha wananchi hao wanatimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi bila hofu,” alisema Bw. Ntwina.
Amesisitiza umuhimu wa Jeshi la Polisi kuepuka migogoro isiyo ya lazima na badala yake kuweka mkazo katika kulinda usalama wa watu na mali zao hasa katika kipindi hiki nyeti cha uchaguzi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Muliro Jumanne, amesema mafunzo hayo yataboresha uwajibikaji, maadili na taaluma miongoni mwa askari polisi.
“Kimsingi mafunzo haya yanatukumbusha kulinda na kuheshimu haki za binadamu na jinsi ambavyo utekelezaji wa sheria unaweza kufanyika katika mazingira yaliyo salama,” alisema Kamanda Muliro.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa kila raia na msimamizi wa sheria kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria za nchi, ili kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa amani na usawa.
No comments:
Post a Comment