HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 2, 2025

Postive Cooker wahamasisha Utumiaji wa Majiko ya Umeme kupikia


Na Mwandishi Wetu.

KAMPUNI ya Positive Cooker imeunga mkono juhudi za Serikali za kuondoa matumizi ya nishati chafu ya kupikia kwa kuendesha kampeni ya elimu kwa wananchi wa Dodoma juu ya matumizi ya majiko janja yanayotumia umeme katika kupikia.

Akizungumza katika kampeni hiyo leo Septemba 2,2025 jijini Dodoma Meneja wa Positive Cooker Kanda ya Kati, Bw. Eliud Swai, amesema lengo ni kuhamasisha wananchi kutumia majiko janja ya umeme kupikia, ikiwa ni sehemu ya mchango wa kampuni hiyo katika kuunga mkono ajenda ya kitaifa ya matumizi ya nishati safi.

Bw. Swai amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuwashawishi Watanzania kuachana na mila potofu kuhusu matumizi ya umeme kupikia na badala yake kuanza kuamini kuwa ni nishati rafiki, nafuu na salama.

“Lengo letu ni kufanya kampeni ya kutunza mazingira. Tunahamasisha wananchi watumie umeme kwa sababu hivi sasa kila nyumba ya Mtanzania ina umeme, lakini wengi wanauhusisha zaidi na mwanga, friji au kuchaji simu. Tunataka watambue kuwa umeme ni nishati nafuu jikoni kwako,” amesema Bw. Swai

Aidha amebainisha kuwa majiko hayo janja yanatumia wastani wa nusu uniti hadi uniti moja kwa saa moja ya kupika, sawa na shilingi 180 hadi 350, hali inayothibitisha ufanisi wake wa gharama.

Hata hivyo amesema kuwa ujio wa teknolojia hiyo mpya utasaidia kuondoa utegemezi wa mkaa na kuni, hivyo kulinda afya za watumiaji na kuokoa misitu.

“Lengo letu ni kutoa elimu kwa kila Mtanzania ili aache kutumia mkaa na kuni. Hii ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono kampeni ya nishati safi ya kupikia na kumsaidia mama wa nyumbani apike bila kero wala gharama kubwa kwa kutumia majiko ya umeme,” ameongeza Bw. Swai.

Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria kampeni hiyo wamesema kuwa elimu waliyopewa imekuwa ya msaada mkubwa, ikiwakumbusha madhara ya matumizi ya nishati chafu na faida za kutumia umeme kupikia.

“Elimu tuliyopewa ni nzuri, inatukumbusha umuhimu wa kutumia majiko haya ya umeme. Zamani tulipokuwa tunatumia kuni na mkaa tulipata changamoto nyingi, ikiwemo kuchelewa kuiva kwa chakula, lakini sasa majiko janja yanaongeza kasi na urahisi wa kupika,” wamesema

Iwapo familia nyingi zitatumia majiko hayo, kasi ya ukataji miti itapungua na hivyo kuimarisha uhifadhi wa misitu, hatua itakayosaidia Tanzania kufikia malengo yake ya kupunguza hewa ya ukaa.    

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad